Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemkamata Askofu
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), baada ya kushuka katika ndege ya
Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) akitokea nchini Kenya.
Askofu Gwajima, alikamatwa jana asubuhi na makachero wa Jeshi la
Polisi waliokuwa wamepiga kambi eneo hilo, baada ya kupata taarifa za
kuwasili kwake.
Vyanzo vya habari kutoka kwa watu wa karibu na Askofu Gwajima,
vilisema kuwa baada ya kiongozi huyo wa kiroho kushuka katika ndege,
alitakiwa kupanda helikopta yake ili aelekee Hoteli ya Sea Cliff iliyopo
Masaki, Dar es Salaam kwa ajili ya mapumziko.
Kabla ya kuanza safari ya kuelekea Sea Cliff, Askofu Gwajima,
alijikuta akiishia mikononi mwa polisi na kupelekwa moja kwa moja Kituo
Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa
Vyanzo hivyo vilidai kuwa baada ya kufikishwa kituoni, alipelekwa kwa
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon
Sirro na baadaye ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo, Camillus
Wambura.
“Askofu Gwajima alikamatwa uwanja wa ndege na polisi akitokea nje ya
nchi na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu na kuhojiwa,
lakini ameachiwa kwa dhamana na simu zake za kiganjani zinashikiliwa
kwa ajili ya uchunguzi,” kilisema chanzo hicho.
Msemaji wa kiongozi huyo wa kiroho, Yekonia Behagaze, alikiri kiongozi wao kukamatwa.
“Ni kweli Askofu Gwajima amekamatwa na polisi leo (jana) asubuhi akitokea nje ya nchi, alihojiwa kwa saa nne,” alisema.
Alisema baada ya kumaliza mahojiano hayo, aliachiwa kwa dhamana ili aendelee na majukumu yake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Sirro, alithibitisha kukamatwa kwa Askofu Gwajima.
“Ameletwa, amehojiwa, amepewa dhamana na uchunguzi unaendelea,” alisema.
Chanzo: Mtanzania.
0 comments:
Post a Comment