Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2016/17 inatarajiwa kuanza
Jumamosi Agosti 20, 2016 kwa michezo mitano huku Bingwa Mtetezi wa Kombe
hilo 2015/16, Young Africans ya Dar es Salaam ikisubiri hadi Agosti 31,
2016 kuanza kutetea taji lake.
Young Africans inatarajiwa kusafiri kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC), kucheza na TP Mazembe kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho
unaotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.
Michezo itakayochezwa kesho ni pamoja na Simba SC itakayoikaribisha
Ndanda FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Taifa, ulioko Chang’ombe Dar es
Salaam, katika mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni wakati Azam itakuwa
mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Azam FC ulioko
Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji.
Kadhalika Stand United ya Shinyanga itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya
Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga sawa na Mtibwa
Sugar itakayoikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Manungu
uliuoko Turiani, Mvomero mkoani Morogoro wakati Prisons ya Mbeya
itasafiri hadi Uwanja wa Majimaji ya Songea kucheza na Majimaji FC ya
huko.
Wakati ligi ikianza, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
linaonya timu kuchezesha wachezaji wa kigeni kama hawana vibali vya
kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi husika kwa
mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Vibali vya kuishi na kufanya kazi vinatolewa na Idara ya Uhamiaji
Tanzania (Uhamiaji) wakati leseni ya kucheza inatolewa na TFF. Vilevile
tumeziagiza klabu kulipia ada za ushiriki kwa kila timu; leseni za
wachezaji, ada za wachezaji na ada za mikataba. Mchezaji hatapewa leseni
ya kucheza kama uongozi wa timu hautakamilisha taratibu za malipo.
TFF linapenda kuzikumbusha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara kwamba hatutatoa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu
haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii ni kwa mujibu wa
kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la
2016/2017.
Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili
kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF
iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji,
watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF.
Ni matarajio yetu kuwa kila
klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na
mchezaji na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano.
0 comments:
Post a Comment