728x90 AdSpace

  • Latest News

    Wednesday, December 30, 2015

    Kutana Na Makala Yaliyoandikwa Na Mh Zitto Kabwe.



    Nimeamka asubuhi saa moja. Rafiki yangu na makamu mwenyekiti wa kamati ya Hesabu za Serikali ( PAC ) kaja kunikumbusha kazi za siku ya ijumaa tarehe 20 Machi 2015; Kupitia taarifa ya CAG kuhusu ukaguzi maalumu wa mfuko wa PPF na kushauriana na Waziri wa Fedha kuhusu Bajeti ya Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa. Tukakubaliana kwamba yeye akaongoze kikao cha PPF na Mimi nitakuwapo kwenye kikao cha Bajeti ya CAG.



    Nikajiandaa kwenda bungeni kupata kifungua kinywa nikiwa na nguo zisizo rasmi. Kwa kuwa tayari taarifa yangu ya kutii uamuzi wa CHADEMA kunifukuza ilikuwa imesambaa kwenye mitandao ya kijamii na gazeti la Nipashe kuiandika yote, wabunge wengi walikuwa wakiniuliza kama tayari nimeshajiuzulu. Nikawaambia hapana bado nipo kazini. 

    Niliporudi nyumbani, nilivalia kanzu yangu ya buluu mpauko na koti la buluu. Sikuwa na kofia, hivyo nikaazima kwa ndugu Juma Nkamia ambaye ninaishi naye jirani katika nyumba za NHC Medeli. Ilikuwa siku ya ijumaa hivyo nilijiweka tayari kwa ajili ya sala ya ijumaa.
    Nikaenda ofisi za Bunge kuonana na Spika ili kukubaliana kuhusu ombi langu la kuzungumza ndani ya Bunge. Kisha nikaenda kuandika barua yangu ya kung'atuka ubunge katika chumba namba 321, chumba cha makatibu wa kamati za LAAC na PAC. Ezekiel Kamwaga na Dickson Bisile walikuwa nami. Bisile alinisaidia kumalizia hotuba nitakayotoa bungeni jioni ile ( ambayo kutokana na muda, usiku mwingi tayari, sikuisoma ).
    Baada ya sala ya ijumaa nilikwenda jengo la Hazina Dodoma ambapo kikao cha PAC kilikuwa kinafanyika. Tayari maafisa wa CAG akiwemo Prof. Mussa Assad walikuwa wameketi na baada ya muda kidogo Waziri wa Fedha Bi. Saada Mkuya Salum aliingia. Tulibishana kidogo kuhusu kwamba CAG ni Afisa wa Serikali au wa Bunge, yeye akisema ni timu yake. Kisheria CAG ni Afisa wa Bunge na sio Sehemu ya Hazina. Kisha nikamtoa nje ili aje na maafisa wake wengine. Katibu Mkuu Bwana Likwelile alikuja. Kikao kikaanza.
    Mjadala mkali ulikuwa kuhusu mtiririko wa fedha kwenda kwa CAG. Sheria ya ukaguzi wa umma kifungu cha 41 na 44 kinataka PAC ikishapitisha Bajeti ya CAG kwa mashauriano na Waziri wa Fedha, Bajeti ile itolewe yote mara moja kwenda mfuko wa Ukaguzi kutoka mfuko Mkuu wa Hazina. Kutokana na upatikanaji wa Mapato ya Serikali, mwaka 2011, PAC ilikubaliana na Serikali kutoa fedha mara 2 kwa mwaka. Nayo ikawa ngumu tukakubaliana kurekebisha na ikawa mara 4 kwa mwaka. Nayo haikukutekelezwa, fedha zikawa zinatoka kwa wiki mbili mbili. Hali hii imeathiri sana utendaji wa ofisi ya CAG kiasi cha CAG kushindwa hata kununua tairi Mpya za gari yake ya kazi. 


    Baada ya mjadala mkali na umuhimu wa kutekeleza Sheria, PAC ilikubaliana na Waziri wa Fedha kutoa fedha za Bajeti ya CAG kwa miezi Sita Sita kwa kutoa 50% mwanzo wa mwaka wa Bajeti na 50% nyingine kila mwezi Januari. Utaratibu huu utaanza katika mwaka wa fedha wa 2015/2016.


    Baada ya hapo tukajadiliana kuhusu Bajeti. Waziri wa Fedha aliomba Bajeti ibakie ile ile ya mwaka Jana wakati CAG kaomba nyongeza ya 21%. Waziri alijulisha kamati kuwa Bajeti ya mwaka 2015/16 kila Wizara na Idara Bajeti imekatwa kwa 19%, hivyo haitakuwa sawa kwa CAG kuongezewa. Waziri aliijulisha kamati kuwa katika Bajeti inayokuja Serikali inataka kujitegemea kwa 100%, bila misaada ya wafadhili. Ndio maana kuna punguzo la Bajeti. 


    PAC ilijenga hoja kwamba CAG anaanza ukaguzi wa mapato ( revenue audit ) na ukaguzi wa mikataba ya Gesi, Mafuta na Madini hivyo kwa mawanda mapya lazima Bajeti iongezeke. Baada ya mjadala tukakubaliana Bajeti ya CAG kupanda kwa 8% kutoka tshs 86 bilioni mpaka tshs 94 bilioni. 

    Watumishi wa CAG walinifuata baada ya kikao na mmoja aliniambia ' tunashukuru kwa kuacha ofisi ikiwa imara. Umetusaidia sana '. Niliwashukuru kwa kazi iliyotukuka katika kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma. 


    Nilikwenda nyumbani kubadili nguo na kuvaa safari suti yangu rangi ya udongo ninayoipenda kuliko zote. Baada ya mashauriano na Wakili Msomi Albert Msando kuhusu barua ya kung'atuka nilikwenda ndani ya ukumbi wa Bunge kwa mara ya mwisho katika bunge la Kumi. Niliwasilisha barua yangu kwa Spika. Nikaingia ukumbini.
    Nilishiriki katika mjadala wa muswada wa sheria ya maafa ngazi ya Kamati ya Bunge zima. Baada ya muswada kumalizika kupitia vifungu mwenyekiti wa Bunge aliniita kuzungumza.
    Sikusoma hotuba niliyoandaa. Nilipata uzito kidogo mwanzoni nikiwatazama wenzangu mule ndani. Kisha nikapata nguvu, nikawaaga.
    Nafurahi nilifanya kazi mpaka dakika ya mwisho kabla ya kung'atuka. 


    ( post inayofuata ni Hotuba yangu ya kuaga Bunge la 10 )

    #‎UlikuwaMwaka2015 Siku yangu ya mwisho Bunge la Kumi Zitto Kabwe
    [ Makala hii niliandika 20.3.2015 ]


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Kutana Na Makala Yaliyoandikwa Na Mh Zitto Kabwe. Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top