728x90 AdSpace

  • Latest News

    Monday, June 6, 2016

    Mitandao ya Kijamii ni umaskini kwa Tanzania?


    Katika miji ya Tanzania leo hii kila kona unayokwenda utaona simu za mkononi zenye uwezo wa kutumia intaneti, almaarufu kama ‘smartphone’, zimezagaa. 

    Kwa mujibu wa jarida la Reuters, watumiaji wa simu za mkononi Tanzania wameongezeka kwa asilimia 16 mwaka 2014 na kufikia watu milioni 31.86 huku watumiaji wa intaneti wakiongezeka kwa asilimia 22 na kufikia watu milioni 11.35 mwaka 2014. Hii idhihirisha sekta ya mawasiliano inakua kwa kasi kubwa. 

    Lakini ni kwa namna gani mitandao ya kijamii ni umaskini kwa Tanzania ilihali inachingia katika pato la taifa? 

    Mwanazuoni nguli Dk. Abunuasi Mwami wakati fulani alishawahi kuniambia kuwa “One physical phenomenon cannot cause another physical phenomenon” (tukio moja la kuonekana haliwezi kuleteleza tukio lingine la kuonekana). 

    Mfano; mtu akinywa maji inatarijwa baada ya muda fulani atatoa haja ndogo, lakini je, ni tendo la kunywa maji linaloleta haja ndogo au ni matokeo ya hali zisizoonekana ambazo huendelea katika mwili wa binadamu ambapo mwishowe huleta haja ndogo? 

    Mfano huu unaeleza ya kuwa ujio wa utandawazi nchini kwetu siyo jambo jema kama vile ambavyo wengi wetu tumekuwa tukiliona na kulishupalia. 

    Utandawazi umechangia kurudisha nyuma maendeleo yetu japokuwa takwimu za wachumi zinaonyesha uwepo wa utandawazi umeleta maendeleo kwa kiasi kikubwa. 

    Tumeshuhudia namna ambavyo mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, instagram, whatsapp, snapchart, tango na mingine mingi ikianzishwa kila uchao na wataalamu mbalimbali wa mawasiliano duniani. 

    Mitandao hii ya kijamii inaendelea kuwa changamoto kwa rasilimali-watu hususan vijana ambao wengi wetu tumeikumbatia na kuifanya sehemu muhimu na ya ulazima katika maisha yetu. Wapo ambao wamejijengea mtazamo kwamba hawawezi kabisa kuishi bila mitandao hiyo. 

    Hebu turejee historia kidogo ili tukumbuke tulikotoka na tuweze kuhusisha na kile ambacho kinaendelea kwa sasa. Tusifikiri yale yanayotokea sasa hivi yamekuja tu bila kuwa na chanzo maalum. 

    Katika karne ya 19 hadi mwanzoni mwa karne ya 20, Bara la Afrika lilitawaliwa na watu kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na Uarabuni. Wakati wa ukoloni ili mabwana wakubwa hao waweze kutimiza lengo lao iliwapasa kwanza kututawala kifikra ili kuonyesha yale tunayoyafanya siyo ya msingi na kuwa ni mambo yasiyostaarabika na ya kichawi. 

    Ikumbukwe kwamba, walivyoanza kuja mabwana wakubwa hawa Afrika walitanguliza wamisionari ili waje kutulegeza kwa jina la kuleta ustaarabu na kutuletea Neno la Mungu kwani waliogopa mkinzano. 

    Ni muhimu kufahamu ili uweze kumtawala mtu kwa urahisi ni lazima kwanza uanze kuiteka fikra yake ili muweze kuyaona mambo katika sura moja, ndiyo maana kuanzia hapa ikawa rahisi kuwatumikisha mababu zetu katika mashamba makubwa kwa kuwaaminisha katika kilimo cha biashara na kuacha kilimo cha mazao ya chakula. Ukoloni huu ulizaa utumwa na mateso ya nguvu kwa Waafrika mpaka pale miaka ya 1940 ambapo biashara ya utumwa ilitangazwa kukoma duniani. 

    Ukoloni huu haukuishia hapa, kwani baada ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru wao ndipo ukoloni mambo-leo ukaanza. Baada ya uhuru nchi nyingi za Afrika zilijua ya kuwa sasa wako huru kufanya yale wayatakayo kama nchi kumbe ilikuwa ni muda wa kupitia upande mwingine wa sarafu iitwayo ‘ubepari’ (Capitalism). 

    Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani walifanya juhudi zote kueneza ubepari huu katika nchi zote za Afrika ili kuzitawala upya bila kuuonyesha uwepo wao moja kwa moja. 

    Ubepari huu ulisambazwa kwa njia ya mashirika ya kimataifa pamoja na Benki ya Dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (International Monetary Fund-IMF). Mashirika haya yalitunga sera mbalimbali ambazo nchi za Afrika na nyingizo walipaswa kuzifuata kwa kisingizio cha kuwatoa kwenye dimbwi la umaskini. Isitoshe sera hizi kutoka kwa mabepari zilikuwa na masharti endapo zisipofuatwa misaada ya mali na pesa isingeletwa. 

    Kwa kuwa nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zilikuwa na shida ikatupaswa kuitikia wito wa mabwana wakubwa na kufungulia soko huria kuanzia miaka ya 1980 tukasahau na kuuona ujamaa kuwa ni mambo ya kishenzi. 

    Huu ulikuwa muendelezo wa kutawaliwa kifikra ambapo ulitufanya kuona bila kupata misaada kutoka kwa mataifa ya kibepari hatuwezi kuendelea na ndipo hapo utegemezi uliokidhiri ulizidi na kuanza kuagiza kila kitu kutoka nje tukigeuka kuwa soko la bidhaa kutoka mataifa ya kibeberu wakati malighafi zote walichukua kwetu bila wenyewe kunufaika. 

    Kama vile haitoshi, utandawazi ukabisha hodi na kuingia, kwa kuwa Tanzania na nchi zingine za Afrika tulishazoea kupokea tu na tulishaaminishwa katika fikra zetu kila kitu kutoka Magharibi ni kizuri. 

    Mbaya zaidi, mabepari hao wakasema ni vigumu kuishi nje ya utandawazi kwani mfumo huo umefanya nchi zote kuwa karibu kama vile watu waishio kijijini. Inatia simanzi kuona vile ambavyo tulizidi kuaminishwa vitu na tukihoji tunaambiwa misaada itasitishwa. 

    Mabepari hawa walitaka tuendelee kufuata wasemayo ili waweze kututawala na ili kufanikisha azma yao hiyo ikaletwa lugha mpya iitwayo ‘Haki za Binadamu’ wakisititiza mtu yeyote yuko huru kufanya kile atakacho. Haki hizi zilipata tafsiri kutoka nchi za kibepari na zikasambazwa kwa kasi kwa kutumia mashirika ya kimataifa yakisaidiwa kwa karibu na asasi zisizo za kiserikali (NGOs). 

    Hivi tulishawahi kujiuliza haki za binadamu wa Kitanzania ni zipi? Au tafsiri tuliyonayo ni kutoka kwa Umoja wa Mataifa? 

    Je, mabepari wa sasa hawatawali fikra kwa kupitia mitandao ya kijamii? Kwanini basi mabepari hao huanzia kwenye fikra zetu? Jibu ni rahisi, Haki za Binadamu! Wanataka ukianza kuhoji wakwambie mtu ana uhuru wa kuamua afanye nini na aache nini. 

    Na ndiyo maana hata leo ukijaribu kuwauliza vijana walio wengi mitaani iweje leo mnatumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kuunufaisha umma mambo yako binafsi ambayo hata yale watu wasingepaswa kujua watakwambia tuna haki kama binadamu kuchagua yale tufanyayo. 

    Leo hii tunashuhudia watu mbalimbali katika mitandao ya kijamii wakieleza umma kuhusu mahusiano yao na wenza wao, wakionyesha sehemu mbalimbali za miili yao, kueleza matatizo yao binafsi kwa jina la kutaka ushauri na wengine kudiriki kurusha picha zao za ngono katika mitandao hiyo kwa kisingizio cha Haki za Binadamu. 

    Tukiangalia kwa uwazi kabisa sharti la ubepari ni kuhakikisha kuwa wanapata faida kubwa kwa kupitia wanyonge ambao hutumikishwa ili kuleta faida kubwa kwa mabepari hao. 

    Hebu tuanze na upande wa kwanza wa unyonywaji, tulishawahi kujiuliza gharama ya kutumia simu ya kawaida isiyokuwa na intaneti na ile iliyo na intaneti (smartphone). Labda ndiyo ama hapana, ila ukiwa na simu ya tochi unahitaji vocha kwa ajili ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno na kupiga japo gharama yake bado siyo ndogo kwani itakupaswa kuunga aina fulani ya vifurushi ili kuweza kuwasiliana na mitandao mingine na gharama hii hupanda kila kukicha. 

    Na ukiwa na simu yenye uwezo wa intaneti (smartphone) inakuwaje sasa? Hapa kuna tofauti kidogo kwani itakupasa kuwa na fedha kwa ajili ya kupiga, ujumbe mfupi wa kawaida na intaneti. Na ikumbukwe gharama hii ni kubwa kwani wameshakuwekea makundi mbalimbali ambayo unapaswa kuchagua ili kufikia huduma yako. 

    Na usipokuwa na fedha kwenye simu yako, hiyo simu yenye uwezo wa intaneti itakufaa nini? Hapa ndipo utaona watu wakitumia fedha nyingi kuhakikisha wanakuwa na vocha kwenye simu zao kwa ajili ya kuingia kwenye mitandao hii ya kijamii kila siku ili kuweza kupata au kutoa taarifa. 

    Cha ajabu zaidi, kuna watu ambao hawafanyi kazi kama watoto na wanafunzi ambao wanamiliki hizo simu zenye intaneti na huhitaji kuweka vocha kila siku, sijui fedha wanapata wapi au ndiyo kundi jipya la utegemizi linaanza kuja sasa Tanzania? 

    Lakini wanaonufaika na mitandao hii ya kijamii ni kina nani? Je, ni walaji au wazalishaji? Jibu rahisi hapa ni makampuni ya simu ya wawekezaji wa kibepari ndiyo ambayo hunufaika zaidi na mitandao hii ya kijamii na kuwaacha walaji kuwa maskini ama kwenda jela hasa baada ya kutungwa sera mpya ya matumizi ya mitandao mwaka 2015. 

    Sera ya unyonyaji wa kibepari ni kuhakisha unapata faida kutoka kwa wavuja jasho wa hali ya chini mpaka wale wa juu ndio maana leo hii katika makampuni ya simu utaona viwango wa kujiunga kifurushi kinaanzia shilingi 250 wakiamini hata yule mvuja jasho wa hali ya chini kabisa anaweza kumudu. 

    Tujiulize kidogo juu ya unyonyaji huu ambapo wengi wetu yamkini hatuuoni ama tunapuuza. Ni wangapi wetu tunaweza kukaa bila intaneti kwa siku nzima? 

    Kwa kuwa makampuni haya ya kibepari yaligundua hii ni sehemu ya kumfanya mtumiaji kuwa maskini kwani wengi wetu bado tunavuja jasho kila kukicha ila hatufanikiwi, wameanzisha huduma za kukopa pesa ili upate intaneti halafu utalipa pindi uwekapo salio. Je, hii siyo namna ya kuongeza umaskini kwa Mtanzania? 

    Hivi tulishawahi kujiuliza mitandao hii ya kijamii imeasisiwa na nani na kwa manufaa ya nani? Majibu yanaweza kuwa mengi hapa kutokana na kila mtu afikiriavyo. Lakini ili kuufanya ubepari ushamiri kirahisi ulimwenguni hasa nyakati hizi ni lazima kuwe na mfumo wa usambazaji ambao utafanya taarifa fulani kufika sehemu nyingi kwa wakati mmoja. 

    Leo hii tuna aina nyingi ya mitandao ya kijamii ambayo hutupa taarifa nyingi za Kimagharibi ambazo wengi wetu huzifurahia na kuona ndizo zenye tija na kuona zile za kwetu kama zimepitwa na wakati. 

    Leo hii ukiingia mtandao wa Instagram na kuona Kim Kardashian kavaa nywele fulani bandia na kapendeza sana moja kwa moja nasi tunapenda kuwa kama yeye, tunaanza kutafuta hizo nywele zenye thamani kubwa nasi tuwe kama yeye. Japo nywele hizo ukizivaa hazileti tija yoyote kwa maendeleo zaidi ya kutumia fedha nyingi ambayo ulivuja jasho muda mrefu kuipata. Mitandao ya kijamii imeshaonyesha ili uwe wa kisasa ni lazima uvae nguo za namna fulani, uweke nywele za namna fulani, utumie manukato fulani. 

    Ambacho wengi wetu tunasahau sasa ni kwamba, haya makampuni ya kibepari ya nywele bandia, manukato, nguo, pochi, kucha bandia wanatumia watu maarufu kuuza bidhaa zao ili sisi wanyonge tuone ndiyo mambo ya kisasa na kuanza kupapatika nayo mwishowe tunazidi kuwa maskini ilhali wao wakipata utajiri maradufu. 

    Huu ni unyonyaji wa hali ya juu, yatupasa kufikiria upya namna ya maisha yetu na kufanya mambo yenye tija ili kulikomboa taifa letu. Hapa utasikia watu wakisema sasa tufanyaje na ndiyo hali ya dunia inavyokwenda yatupasa kwenda na kasi hiyo. 

    Inatupasa kama taifa kuliona hili ili kuweza kulikomboa kwa kuwa na mijadala kila mahali nchini kwani ukisema tufanye hivi utapata jibu la Haki za Binadamu. 

    Kwa upande mwingine, ili kutengeneza soko zuri kwa mabebari ni sharti kutengeneza taifa tegemezi ambalo litakuwa siyo bunifu na mwishowe kutoa masoko ya uhakika. 

    Sasa hivi Tanzania kama taifa lina vita kubwa ya kupambana dhidi ya mitandao ya kijamii kwani wengi wetu tumesha athirika kiasi kwamba ukikaa dakika mbili mbali na simu yako unajihisi mgonjwa. Tumekuwa walevi wa simu (addicted) kama wenye kutumia madawa ya kulevya au walevi wa pombe ambao hawaendeshi maisha pasi utumiaji wa vileo. 

    Kiuhalisia jaribu kukaa na jamaa zako kama wanne mkiwa mahali katika mazungumzo ya jioni halafu angalia vile watu walivyokuwa karibu na simu zao kiasi kwamba meza inakosa mazungumzo kabisa. Ingawa mkoa pamoja, lakini kila mmoja yuko mbali, amezama kwenye simu na wakati mwingine anaweza kununa ama kuangua kicheko kutegemeana na ujumbe aliousoma kwenye mtandao wa kijamii.

    Siku hizi hata familia nyingi watoto wanakosa uangalizi mzuri kwani wazazi wakirudi nyumbani nao wako karibu na simu zao kuliko vile walivyo karibu na watoto wao. 

    Je, hii siyo aina nyingine ya umaskini? Sehemu muhimu ya maendeleo ya binadamu ni kuhakikisha watu wanakutana pamoja kujadili maendeleo ya nchi yao kwa hoja. 

    Leo sote fikra zetu ziko kwenye kuangalia mitandao ya kijamii na kusahau kufanya mijadala yenye tija kwa taifa letu. 

    Leo hii kukitokea ajali kila mtu anataka kuwa mwandishi wa habari wa kwanza kutoa taarifa ya tukio la ajali badala ya kuanza kuwaokoa majeruhi katika ajali hiyo. 

    Fikra zetu ndizo mkombozi wetu kwani zinatuletea ubunifu katika maisha ili kuweza kufanya mambo yenye tija katika taifa ila kwa kuwa tumeukumbatia ubepari kwa dhati, ubepari huo umeteka fikra zetu kiasi kwamba tunasahau kubuni mambo ya msingi ya jamii zetu na kubaki kuwa walaji wa yale yote yanayoletwa na nchi za Magharibi.

    Mitandao ya kijamii imefanikiwa kuteka fikra zetu na ubunifu wetu na hivi ndivyo Tanzania itaendelea kuwa maskini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Mitandao ya Kijamii ni umaskini kwa Tanzania? Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top