NIKO
kwenye jiji kubwa kuliko yote hapa nchini Uturuki. Mengi yanaweza yakawa
yanajulikana au gumzo, lakini huenda hakuna zaidi ya soka.
Si
unajua Tanzania tunavyopenda soka la England na tunashangilia kwelikweli huku
kila mtu akiwa amejipandika timu yake, hapa sahau.
Wao wana timu zao, wanaziheshimu na kuzipa thamani kubwa kuliko unavyofikiria.
Mambo ya England, wamewaachia Waingereza wenyewe.
Hii
pia ni kutokana na kukua kwa soka la hapa ambalo linatawaliwa na klabu kubwa
tatu za Galatasaray, Fernabahce pamoja na Beskats.
Soka
lao, kweli linapiga hatua. Mambo wanayofanya yamenifanya nikumbuke nyumbani kwa
kuwa nilimsikia Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ akijitamba
kabla ya mechi yake ya kirafiki dhidi ya Simba.
Halafu
baada ya sare, akakumbushia alichokisema kwamba timu yake yenye wazalendo wengi
ina uwezo mkubwa.
Kweli
wameisumbua Simba na kumaliza mechi kwa sare ya bila mabao. Naweza kusema, acha
tumsubiri Julio katika Ligi Kuu Bara.
Pamoja
na hivyo, sikuishia hapo. Muungwana yoyote angependa kujipa maswali na
ikiwezekana kuyajibu kwa haki bila ya kuonea.,
Hivi
huyu Julio, kweli tunapaswa kuamini sifa yake moja tu, kwamba ni mtu wa maneno
mengi sana, kelele nyingi sana na hana lolote.
Pamoja
na maneno yake ambayo huenda ni asili kwake kwa kuwa amekulia uswahilini kama
kwetu, kule Kigogo jijini Dar es Salaam, lakini kazi yake mbona inaonekana.
Aliipandisha
Mwadui FC msimu uliopita kwa maana ya pointi, akaachwa daraja la kwanza kwa
kuwa Stand United walikata rufaa na kushinda.
Ungesema
hesabu ni uwanjani basi yeye alistahili kusonga mbele. Ok, akaapa msimu
unaofuatia atapanda.
Kweli
msimu uliofuatia Mwadui FC ikapanda, tena ikabeba na ubingwa wa daraja la
kwanza kwa kuifunga African Sports.
Usisahau
wakati anaipandisha timu, asilimia kubwa ya wachezaji aliokuwa nao ni wale
walioonekana hawafai kwenye vikosi vingi, mfano mzuri ni Athumani Iddi ‘Chuji’
ambaye alimpa unahodha kabisa.
Hali
inavyokwenda, Julio anakwenda kuwa tishio Ligi Kuu Bara kama hatayumba kupitia
mwendo anaokwenda.
Julio
ni Mtanzania, pamoja na maneno yake, kazi yake bora kabisa inaonekana. Lakini
karibu kila mmoja ametia pamba machoni na vipanzi masikioni asisikie wala kuona
mazuri anayofanya.
Waturuki
wanathamini na kutamani vyao. Hatumpi Julio sifa yake lakini Wazungu wanakuja
nyumbani kwetu, wanalipwa mara tatu nne au tano ya Julio na hawafanyi kama kazi
yake.
Niliwahi
kukumbusha kuhusiana na Julio, kweli ana maneno mengi, kweli ana shombo. Lakini
huyu jamaa ni muhimu sana katika mpira wa Tanzania.
Ana
ya kumlaumu au anaudhi lakini ni changamoto, hakika anaupenda mpira kwa dhati
na ndiyo maisha yake miaka yote.
Sina
haja yoyote ya kutaka kulaumu, lakini nataka niwakumbushe kwamba huyu Julio
tumthamini, tumkubali na tumpongeze kwa kuwa Mtanzania mchapakazi na mwenye
mafanikio kwa mengi anayoyafanya kwenye mpira wa Tanzania.
Tusisubiri
siku ‘akishaondoka’, basi kila mmoja wetu aanza kusambaza sifa zake huku
akieleza mengi mazuri kuhusu yeye.
Hapa Uturuki wanavipenda na kuthamini vyao kwelikweli. Lakini huko nyumbani, hatupendani, hatupendi vyetu na tunapenda ugeni wa kila kitu ili mradi kiwe kinatokea nje ya mipaka ya nchi yetu!
0 comments:
Post a Comment