“KILA raia wa Norway, hata yule ambaye hajazaliwa, ana uhakika wa akiba ya Kroner takriban 600,000
wakati hapa Tanzania pekee, kila mmoja anadaiwa zaidi ya Shs. 700,000
kutokana na Deni la Taifa,” ndivyo anavyosema Profesa Patrick Lumumba,
Mkuu wa Shule ya Sheria ya Kenya.
Profesa Lumumba anasema kwamba, uchumi imara wa Norway unaotokana na
usimamizi madhubuti wa mafuta na gesi, ukichangiwa na idadi ndogo ya
watu ambao asilimia kubwa ni wazalishaji, umeifanya nchi hiyo kuwa mfano
duniani katika ukuzaji wa uchumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni wakati wa semina kuhusu
Masuala ya Mafuta na Gesi iliyoandaliwa na taasisi ya Wajibu – Institute
of Public Accountability (WIPA), Profesa Lumumba alisema uchumi wa nchi
nyingi zinazoendelea hasa barani Afrika ambazo zina rasilimali
mbalimbali unashindwa kukua kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo
uongozi mbovu, rushwa, uzembe pamoja na idadi kubwa ya watu.
Hali hiyo, alisema inazifanya nchi hizo kuwa na mzigo mkubwa wa
kuhudumia watu wake na kushindwa kutoa huduma bora kama elimu, afya na
nyinginezo, hivyo kulazimika kukopa ili kuziba pengo lililopo.
“Norway ina watu milioni 5.2 tu, idadi ambayo ni sawa na wakazi wote wa
Dar es Salaam, lakini uchumi wake ni mkubwa, wameweza kulinda
rasilimali zao na kudhibiti kasi ya kuzaliana ili kuwa na nguvu imara
inayopata huduma zote muhimu.
“Kwa mujibu wa sharia inayosimamia Mfuko Maalum wa mapato ya rasilimali hizo (Government Pension Fund-Global),
serikali imeruhusiwa kuchukua asilimia 4 ya fedha hizo ili kufanya
shughuli nyingine za maendeleo, hususan uwekezaji, lakini kutokana na
kujimudu kiuchumi, ni mwaka jana tu ndipo ilipanga kuchukua kiasi ili
kuwekeza,” alisema Profesa Lumumba.
Kulingana na takwimu zilizopo, Tanzania inaelemewa na mzigo wa deni la Shs. 35.01 trilioni
huku ikijikongoja kukuza uchumi wake, wakati nchi ndogo ya Norway ina
akiba ya Dola 900 bilioni katika Mfuko huo Maalum, ambazo ni takriban
Shs. trilioni 1,939.
Hali hiyo inawafanya raia 5,214,900 wa Norway, nchi inayotegemea uchumi
mkubwa wa mafuta, kuwa na akiba ya wastani wa Dola 173,077 (Shs.
373,028,000) kila mmoja, fedha ambazo zimeanza kuwekwa kwenye mfuko huo
kwa zaidi ya miaka mingi, lengo likiwa kuwekeza kwa vizazi vijavyo
utajiri huo unaotokana na mafuta.
Norway inaamini kwamba, ipo siku mafuta yatakwisha, hivyo wanapaswa
kuweka akiba ya fedha kwa vizazi vijavyo ili navyo vije vinufaike kwamba
nchi yao iliwahi kuwa na rasilimali za mafuta badala ya kusoma kwenye
vitabu kama historia bila kuona manufaa yoyote.
Kutokana na deni linaloikabili Tanzania, wachambuzi wa masuala ya
uchumi na wanasiasa wamekuwa wakisema kwamba, kwa Watanzania milioni 45
waliopo sasa, maana yake kila mmoja anadaiwa Shs. 778,000,
huku utafiti na takwimu ukionyesha kiwango cha umaskini vijijini
kimepungua kwa asilimia 6.1 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Dk. Joel Silas wa Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
anasema kwamba, uwiano wa uchumi na idadi ya watu ni muhimu kuzingatiwa,
kwani ndio unaoweza kupima maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa
ujumla.
Mtaalamu huyo wa uchumi anasema, baadhi ya nchi zimepiga hatua kiuchumi
kutokana na idadi ya watu na rasilimali zilizopo, na kusisitiza kwamba
uzazi wa mpango ndiyo njia pekee inayoweza kufanikisha jitihada za
mataifa yanayoendelea kujikwamua kiuchumi.
“Huwezi kuzungumzia maendeleo bila kutazama idadi ya watu, hata
nyumbani, chakula kinapikwa kulingana na watu waliopo, wakati mwingine
katika hali ya umaskini, inalazimu watu waliopo, hata kama watakuwa
wengi, wagawane chakula hicho hata kikiwa kidogo – ndiyo hali
inayozikabili nchi zinazoendelea ambazo zinashindwa kukidhi mahitaji ya
watu wake na kulazimika kukopa,” anasema.
Ingawa Tanzania inajivunia kugunduliwa kwa uchumi mpya wa gesi na
mafuta, lakini hauwezi kusaidia ikiwa kasi ya ongezeko la watu
haitapungua, huku idadi kubwa wakiwa tegemezi.
Wakati Tanzania yenye ukubwa wa kilometa za mraba 947,303 na idadi ya
watu milioni 45, ni watu milioni 25.59 tu wanaofanya kazi na kuzalisha,
ikizidiwa kwa mbali na Norway ambayo kati ya watu milioni 5.2, karibu
watu milioni 3 (sawa na asilimia 69) wenye umri kati ya miaka 15-74
wanafanya kazi.
Aidha, Pato la Taifa la Tanzania (GDP) nalo liko chini (Dola 48.06
bilioni) huku kipato cha mwananchi mmoja mmoja kikiwa Dola 768, wakati
GDP ya Norway ni Dola 363.290 bilioni na kipato cha mwananchi mmoja ni
Dola 69,712 kwa mwaka.
Ongezeko la idadi ya watu duniani, ambalo linachangiwa na mambo mengi,
yakiwemo ukosefu elimu na huduma za uzazi wa mpango, linatajwa kuwa
janga linalokwamisha hata Malengo Endelevu ya Dunia.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, idadi ya watu duniani inaongezeka kwa watu 200,000 kila siku huku asilimia kubwa ikiwa ni katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Katika kipindi cha miaka 20 kati yam waka 1980 na 2000 idadi ya watu
duniani iliongezeka kutoka bilioni 4.4 hadi watu bilioni 6, huku
asilimia 85 ya ongezeko hilo ikitokea katika nchi maskini na
zinazoendelea.
Kupungua kwa idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi katika miongo kadhaa,
kumesaidia kuongeza idadi ya watu lakini kumekuwa changamoto kubwa
katika uchumi wa mataifa mbalimbali kutokana na kusababisha uhaba wa
ajira pamoja na huduma nyingine muhimu za kijamii.
Mahitaji muhimu kama chakula, huduma za afya, elimu, makazi, ardhi,
ajira na nishati yanakumbwa na changamoto kubwa kwenye mataifa
yanayoendelea ambayo uchumi wake unajikongoja.
Mnamo Septemba 25, 2015, nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa
ziliridhia malengo 17 kwa nia ya kutokomeza umaskini, kulinda sayari
dunia, kudumisha ustawi kwa wote ikiwa ni sehemu ya agenda ya maendeleo
endelevu ambapo kila lengo limepangiwa kukamilika katika kipindi cha
miaka 15 ijayo.
Ili kuyafikia malengo hayo, serikali, sekta binafsi, taasisi za kijamii
na jamii kwa ujumla inapaswa kushiriki kikamilifu katika njia zote
ambazo zinaweza kuleta tija, lakini suala la uzazi wa mpango likipaswa
kupewa kipaumbele.
1. Kutokomeza kabisa umaskini wa namna zote
2. Kutokomeza njaa, kuhifadhi chakula na kuboresha lishe pamoja na kuhimiza kilimo endelevu
3. Kuhakikisha maisha bora na kudumisha ustawi wa wote katika kila umri
4. Kuhakikisha ushirikishwaji na upatikanaji wa elimu bora pamoja na kudumisha fursa za kujifunzia kwa wote
5. Kufikia usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana
6. Kuhakikisha upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na mazingira
7. Kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya gharama nafuu, ya uhakika, endelevu na ya kisasa kwa wote
8. Kudumisha ukuaji endelevu wa uchumi wenye ushirikishwaji, na ajira za kudumu na zenye tija kwa watu wote
9. Kujenga miundombinu bora, kudumisha ushirkishwaji wa maendeleo endelevu ya viwanda na kuchochea ubunifu
10. Kupunguza matabaka ndani na miongoni mwa nchi zote
11. Kuyafanya majiji na makazi ya watu kuwa ya ushirikishwaji, salama, bora na endelevu
12. Kuhakikisha uwiano sawa wa uzalishaji na matumizi
13. Kuchukua hatua za dharura kupambana na mabadiliko wa mazingira na athari zake
14. Kutunza na kusimamia matumizi endelevu ya bahari na rasilimali za majini kwa maendeleo endelevu
15. Kulinda, kuhuisha na kudumisha matumizi endelevu ya vyanzo vya
maji, usimamizi endelevu wa misitu, kukabiliana na hatari ya jangwa, na
kukomesha na kutunza ardhi ili kuokoa viumbe hai
16. Kudumisha Amani na kushirikisha jamii kwa maendeleo endelevu,
kudumisha upatikanaji wa haki kwa wote na kujenga taasisi imara na
zinazowajibika katika ngazi zote
17. Kuimarisha njia za utekelezaji na kutoa kipaumbele cha Ushirikiano wa Dunia kwa Maendeleo Endelevu
0 comments:
Post a Comment