Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17
maarufu kama Serengeti Boys, Bakari Shime amesema hana wasiwasi kuwavaa
India-wenyeji wa michuano maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF
Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo
(AIFF).
Shime ambaye kikosi chake kilitoka sare ya 1-1 na Marekani Jumapili
ya Mei 15, 2016, kesho Jumanne kikosi chake kitawavaa India kwenye
Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco jijini Goa kabla ya kuahidi kuwatungua
wenyeji hao kwenye michuano hiyo inayofanyika ikiwa ni kuipa baraka
India kabla ya fainali za kombe la Dunia kwa vijana mwakani-2017.
Katika mchezo wa Jumapili Marekani ndio walioanza kutangulia kufunga
bao dakika ya tano lililowekwa kimiani na Jean Julien wakati bao la
kusawazisha la Serengeti lilifungwa na Mohammed Abdallah katika dakika
ya 16.
Kwa mujibu wa ratiba, Serengeti Boys itacheza mchezo wake wa tatu
dhidi ya Korea Kusini Mei 19, 2016 kabla ya kumalizia na Malaysia Mei
21, 2016. Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 na kabla ya mchezo
wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo
Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.
Katika historia ya soka duniani, AIFF imeipa Tanzania heshima
kuialika kwenye michuano hiyo ukiacha nyingine nyingine za Afrika zenye
mafanikio makubwa ya soka kwa kuipa nafasi Serengeti Boys ambayo
inalelewa na Shirikisho la Soka Tanzania chini ya uongozi wa Rais Jamal
Malinzi.
Mashindano hayo ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ni sehemu ya
maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa
Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.
Kikosi cha Serengeti:
Kikosi hicho cha wachezaji 22, kiko chini ya Kocha Bakari Shime na
kinaundwa na makipa, Ramadhan Kabwili, Kelvin Kayego na Samwel Brazio
wakati mabeki wa pembeni ni Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel
Mwenda na Ally Msengi.
Mabeki wa kati ni Issa Makamba, Nickson Job na Ally Ng’anzi huku
viungo wakiwa ni Maulid Lembe, Asad Juma, Kelvin Naftari, Yasin Mohamed
na Syprian Mwetesigwa na washambuliaji ni Aman Maziku, Rashid Chambo,
Enrick Nkosi, Yohana Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na Muhsin
Mkame.
Maofisa watakaosafiri na timu hiyo ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji wa TFF, Ayoub Nyenzi, Mshauri wa ufundi wa timu za vijana, Kim
Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime, Kocha wa Makipa Mohamed Muharami,
Daktari wa timu, Shecky Mngazija na mtunza vifaa, Edward Edward.
0 comments:
Post a Comment