SEHEMU mbalimbali duniani wanawake wanatarajiwa kuishi umri mkubwa
ikilinganishwa na wanaume. Kimsingi,
watu wengi wana bibi zao kuliko babu zao.
Kwanini
iko hivi na ni nini husababisha? Kulingana na utafiti uliofanywa na Chuo
Kikuu cha Southern California nchini Marekani, watafiti wa masuala ya jamii,
saikolojia na utambuzi kuhusu kuzeeka wanadai tofauti za umri wa kuishi kati ya
jinsia hizi zilianza mwanzoni mwa karne ya 20.
Mapinduzi ya viwanda katika nchi zilizoendelea,
hasa za Ulaya na Amerika yalipelekea kuwepo kwa njia bora za kuzuia magonjwa,
lishe bora na tabia nzuri ya kulinda afya ambapo katika miaka ya 1800 na mwanzoni
mwa 1900 yalichangia kupungua kwa vifo, wakati huo huo jinsia ya kike kuongeza
umri wa kuishi kwa kasi kubwa.
Katika miaka ya sasa, kumekuwa na upungufu mkubwa wa vifo uliotawanyika,
mapitio ya takwimu za dunia yanaonyesha kwamba magonjwa ya moyo kwa watu wazima
ndiyo chanzo kikuu cha vifo kwa wanaume kulingana na maprofesa kutoka Chuo
Kikuu cha Southern California na AARP.
“Tunashangazwa na tofauti kubwa ya vifo kati ya wanaume na wanawake
iliyoanza mwanzoni mwa miaka ya 1870,” maprofesa hao walisema.
Utafiti huo ulifanywa na William F. Kieschnick, Profesa wa Chuo Kikuu cha
Southern California katika masuala ya baiolojia ya kuzeeka na Hiram
Beltrán-Sánchez, mtafiti wa Kituo cha Demografia ya Afya na Kuzeeka wa Chuo
Kikuu cha Wisconsin-Madison. Utafiti huo ulihusisha watu walioishi kati ya
miaka ya 1800 na 1935 katika nchi 13 zilizoendelea.
Maprofesa hao walichunguza vifo vya watu wazima kuanzia miaka 40,
ambapo timu hiyo ya watafiti iligundua watu waliozaliwa baada ya 1880, kiwango
cha vifo vya wanawake kilipungua kwa asilimia 70 haraka zaidi ya wanaume.
Hata baada ya kudhibiti vifo vinavyotokana na uvutaji sigara, bado magonjwa
ya moyo yalionekana kuwa sababu kubwa ya vifo vya wanaume wenye zaidi ya miaka
40. Inashangaza uvutaji wa sigara ulichangia asilimia 30 ya tofauti ya vifo
kati ya jinsia hizo baada ya 1890.
Athari isiyolingana ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo kwa wanaume
hasa kipindi cha kati na mwanzoni mwa uzee, inaibua swali je, wanaume na
wanawake wanapatwa na hatari za magonjwa ya moyo kwa namna tofauti? Je, ni
kutokana na kurithi au mambo mengine yanayowalinda katika maisha yao?
Watafiti hao walisema, tafiti zijazo zitajumuisha uchambuzi wa vyakula na
tofauti ya mazoezi katika nchi mbalimbali, uchunguzi wa kina wa chembe za
urithi kati ya jinsia zote pamoja na uhusiano wa matokeo hayo kwenye afya ya
ubongo katika umri mkubwa ili kujua nini hasa kinawafanya wanawake waishi
maisha marefu zaidi ya wanaume.
0 comments:
Post a Comment