Katika miji ya Tanzania leo hii kila kona unayokwenda utaona simu za
mkononi zenye uwezo wa kutumia intaneti, almaarufu kama ‘smartphone’,
zimezagaa.
Kwa mujibu wa jarida la Reuters, watumiaji wa simu za mkononi
Tanzania wameongezeka kwa asilimia 16 mwaka 2014 na kufikia watu milioni
31.86 huku watumiaji wa intaneti wakiongezeka kwa asilimia 22 na
kufikia watu milioni 11.35 mwaka 2014. Hii idhihirisha sekta ya
mawasiliano inakua kwa kasi kubwa.
Lakini ni kwa namna gani mitandao ya kijamii ni umaskini kwa Tanzania ilihali inachingia katika pato la taifa?
Mwanazuoni nguli Dk. Abunuasi Mwami wakati fulani alishawahi kuniambia
kuwa “One physical phenomenon cannot cause another physical phenomenon”
(tukio moja la kuonekana haliwezi kuleteleza tukio lingine la
kuonekana).
Mfano; mtu akinywa maji inatarijwa baada ya muda fulani atatoa haja
ndogo, lakini je, ni tendo la kunywa maji linaloleta haja ndogo au ni
matokeo ya hali zisizoonekana ambazo huendelea katika mwili wa binadamu
ambapo mwishowe huleta haja ndogo?
Mfano huu unaeleza ya kuwa ujio wa utandawazi nchini kwetu siyo jambo
jema kama vile ambavyo wengi wetu tumekuwa tukiliona na kulishupalia.
Utandawazi umechangia kurudisha nyuma maendeleo yetu japokuwa takwimu za wachumi zinaonyesha uwepo wa utandawazi umeleta maendeleo kwa kiasi kikubwa.
Tumeshuhudia namna ambavyo mitandao ya kijamii kama vile facebook, twitter, instagram, whatsapp, snapchart, tango na mingine mingi ikianzishwa kila uchao na wataalamu mbalimbali wa mawasiliano duniani.
Mitandao hii ya kijamii inaendelea kuwa changamoto kwa rasilimali-watu
hususan vijana ambao wengi wetu tumeikumbatia na kuifanya sehemu muhimu
na ya ulazima katika maisha yetu. Wapo ambao wamejijengea mtazamo kwamba
hawawezi kabisa kuishi bila mitandao hiyo.
Hebu turejee historia kidogo ili tukumbuke tulikotoka na tuweze
kuhusisha na kile ambacho kinaendelea kwa sasa. Tusifikiri yale
yanayotokea sasa hivi yamekuja tu bila kuwa na chanzo maalum.
Katika karne ya 19 hadi mwanzoni mwa karne ya 20, Bara la Afrika
lilitawaliwa na watu kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na Uarabuni. Wakati
wa ukoloni ili mabwana wakubwa hao waweze kutimiza lengo lao iliwapasa
kwanza kututawala kifikra ili kuonyesha yale tunayoyafanya siyo ya
msingi na kuwa ni mambo yasiyostaarabika na ya kichawi.
Ikumbukwe kwamba, walivyoanza kuja mabwana wakubwa hawa Afrika
walitanguliza wamisionari ili waje kutulegeza kwa jina la kuleta
ustaarabu na kutuletea Neno la Mungu kwani waliogopa mkinzano.
Ni muhimu kufahamu ili uweze kumtawala mtu kwa urahisi ni lazima kwanza
uanze kuiteka fikra yake ili muweze kuyaona mambo katika sura moja,
ndiyo maana kuanzia hapa ikawa rahisi kuwatumikisha mababu zetu katika
mashamba makubwa kwa kuwaaminisha katika kilimo cha biashara na kuacha
kilimo cha mazao ya chakula. Ukoloni huu ulizaa utumwa na mateso ya
nguvu kwa Waafrika mpaka pale miaka ya 1940 ambapo biashara ya utumwa
ilitangazwa kukoma duniani.
Ukoloni huu haukuishia hapa, kwani baada ya nchi nyingi za Afrika
kupata uhuru wao ndipo ukoloni mambo-leo ukaanza. Baada ya uhuru nchi
nyingi za Afrika zilijua ya kuwa sasa wako huru kufanya yale wayatakayo
kama nchi kumbe ilikuwa ni muda wa kupitia upande mwingine wa sarafu
iitwayo ‘ubepari’ (Capitalism).
Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani walifanya juhudi zote kueneza
ubepari huu katika nchi zote za Afrika ili kuzitawala upya bila
kuuonyesha uwepo wao moja kwa moja.
Ubepari huu ulisambazwa kwa njia ya mashirika ya kimataifa pamoja na
Benki ya Dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (International Monetary
Fund-IMF). Mashirika haya yalitunga sera mbalimbali ambazo nchi za
Afrika na nyingizo walipaswa kuzifuata kwa kisingizio cha kuwatoa kwenye
dimbwi la umaskini. Isitoshe sera hizi kutoka kwa mabepari zilikuwa na
masharti endapo zisipofuatwa misaada ya mali na pesa isingeletwa.
Kwa kuwa nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zilikuwa na shida
ikatupaswa kuitikia wito wa mabwana wakubwa na kufungulia soko huria
kuanzia miaka ya 1980 tukasahau na kuuona ujamaa kuwa ni mambo ya
kishenzi.
Huu ulikuwa muendelezo wa kutawaliwa kifikra ambapo ulitufanya kuona
bila kupata misaada kutoka kwa mataifa ya kibepari hatuwezi kuendelea na
ndipo hapo utegemezi uliokidhiri ulizidi na kuanza kuagiza kila kitu
kutoka nje tukigeuka kuwa soko la bidhaa kutoka mataifa ya kibeberu
wakati malighafi zote walichukua kwetu bila wenyewe kunufaika.
Kama vile haitoshi, utandawazi ukabisha hodi na kuingia, kwa kuwa
Tanzania na nchi zingine za Afrika tulishazoea kupokea tu na
tulishaaminishwa katika fikra zetu kila kitu kutoka Magharibi ni kizuri.
Mbaya zaidi, mabepari hao wakasema ni vigumu kuishi nje ya utandawazi
kwani mfumo huo umefanya nchi zote kuwa karibu kama vile watu waishio
kijijini. Inatia simanzi kuona vile ambavyo tulizidi kuaminishwa vitu na
tukihoji tunaambiwa misaada itasitishwa.
Mabepari hawa walitaka tuendelee kufuata wasemayo ili waweze kututawala
na ili kufanikisha azma yao hiyo ikaletwa lugha mpya iitwayo ‘Haki za
Binadamu’ wakisititiza mtu yeyote yuko huru kufanya kile atakacho. Haki
hizi zilipata tafsiri kutoka nchi za kibepari na zikasambazwa kwa kasi
kwa kutumia mashirika ya kimataifa yakisaidiwa kwa karibu na asasi
zisizo za kiserikali (NGOs).
Hivi tulishawahi kujiuliza haki za binadamu wa Kitanzania ni zipi? Au tafsiri tuliyonayo ni kutoka kwa Umoja wa Mataifa?
Je, mabepari wa sasa hawatawali fikra kwa kupitia mitandao ya kijamii?
Kwanini basi mabepari hao huanzia kwenye fikra zetu? Jibu ni rahisi,
Haki za Binadamu! Wanataka ukianza kuhoji wakwambie mtu ana uhuru wa
kuamua afanye nini na aache nini.
Na ndiyo maana hata leo ukijaribu
kuwauliza vijana walio wengi mitaani iweje leo mnatumia muda mwingi
katika mitandao ya kijamii kuunufaisha umma mambo yako binafsi ambayo
hata yale watu wasingepaswa kujua watakwambia tuna haki kama binadamu
kuchagua yale tufanyayo.
Leo hii tunashuhudia watu mbalimbali katika mitandao ya kijamii wakieleza umma kuhusu mahusiano yao na wenza wao,
wakionyesha sehemu mbalimbali za miili yao, kueleza matatizo yao
binafsi kwa jina la kutaka ushauri na wengine kudiriki kurusha picha zao
za ngono katika mitandao hiyo kwa kisingizio cha Haki za Binadamu.
Tukiangalia kwa uwazi kabisa sharti la ubepari ni kuhakikisha kuwa
wanapata faida kubwa kwa kupitia wanyonge ambao hutumikishwa ili kuleta
faida kubwa kwa mabepari hao.
Hebu tuanze na upande wa kwanza wa unyonywaji, tulishawahi kujiuliza
gharama ya kutumia simu ya kawaida isiyokuwa na intaneti na ile iliyo na
intaneti (smartphone). Labda ndiyo ama hapana, ila ukiwa na simu ya
tochi unahitaji vocha kwa ajili ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno na
kupiga japo gharama yake bado siyo ndogo kwani itakupaswa kuunga aina
fulani ya vifurushi ili kuweza kuwasiliana na mitandao mingine na
gharama hii hupanda kila kukicha.
Na ukiwa na simu yenye uwezo wa intaneti (smartphone) inakuwaje sasa?
Hapa kuna tofauti kidogo kwani itakupasa kuwa na fedha kwa ajili ya
kupiga, ujumbe mfupi wa kawaida na intaneti. Na ikumbukwe gharama hii ni
kubwa kwani wameshakuwekea makundi mbalimbali ambayo unapaswa kuchagua
ili kufikia huduma yako.
Na usipokuwa na fedha kwenye simu yako, hiyo simu yenye uwezo wa
intaneti itakufaa nini? Hapa ndipo utaona watu wakitumia fedha nyingi
kuhakikisha wanakuwa na vocha kwenye simu zao kwa ajili ya kuingia
kwenye mitandao hii ya kijamii kila siku ili kuweza kupata au kutoa
taarifa.
Cha ajabu zaidi, kuna watu ambao hawafanyi kazi kama watoto na
wanafunzi ambao wanamiliki hizo simu zenye intaneti na huhitaji kuweka
vocha kila siku, sijui fedha wanapata wapi au ndiyo kundi jipya la
utegemizi linaanza kuja sasa Tanzania?
Lakini wanaonufaika na mitandao hii ya kijamii ni kina nani?
Je, ni walaji au wazalishaji? Jibu rahisi hapa ni makampuni ya simu ya
wawekezaji wa kibepari ndiyo ambayo hunufaika zaidi na mitandao hii ya
kijamii na kuwaacha walaji kuwa maskini ama kwenda jela hasa baada ya
kutungwa sera mpya ya matumizi ya mitandao mwaka 2015.
Sera ya unyonyaji wa kibepari ni kuhakisha unapata faida kutoka kwa
wavuja jasho wa hali ya chini mpaka wale wa juu ndio maana leo hii
katika makampuni ya simu utaona viwango wa kujiunga kifurushi kinaanzia
shilingi 250 wakiamini hata yule mvuja jasho wa hali ya chini kabisa
anaweza kumudu.
Tujiulize kidogo juu ya unyonyaji huu ambapo wengi wetu yamkini
hatuuoni ama tunapuuza. Ni wangapi wetu tunaweza kukaa bila intaneti kwa
siku nzima?
Kwa kuwa makampuni haya ya kibepari yaligundua hii ni sehemu ya
kumfanya mtumiaji kuwa maskini kwani wengi wetu bado tunavuja jasho kila
kukicha ila hatufanikiwi, wameanzisha huduma za kukopa pesa ili upate
intaneti halafu utalipa pindi uwekapo salio. Je, hii siyo namna ya
kuongeza umaskini kwa Mtanzania?
Hivi tulishawahi kujiuliza mitandao hii ya kijamii imeasisiwa na nani
na kwa manufaa ya nani? Majibu yanaweza kuwa mengi hapa kutokana na kila
mtu afikiriavyo. Lakini ili kuufanya ubepari ushamiri kirahisi
ulimwenguni hasa nyakati hizi ni lazima kuwe na mfumo wa usambazaji
ambao utafanya taarifa fulani kufika sehemu nyingi kwa wakati mmoja.
Leo hii tuna aina nyingi ya mitandao ya kijamii ambayo hutupa taarifa
nyingi za Kimagharibi ambazo wengi wetu huzifurahia na kuona ndizo zenye
tija na kuona zile za kwetu kama zimepitwa na wakati.
Leo hii ukiingia mtandao wa Instagram na kuona Kim Kardashian kavaa nywele fulani bandia
na kapendeza sana moja kwa moja nasi tunapenda kuwa kama yeye, tunaanza
kutafuta hizo nywele zenye thamani kubwa nasi tuwe kama yeye. Japo
nywele hizo ukizivaa hazileti tija yoyote kwa maendeleo zaidi ya kutumia
fedha nyingi ambayo ulivuja jasho muda mrefu kuipata. Mitandao ya
kijamii imeshaonyesha ili uwe wa kisasa ni lazima uvae nguo za namna
fulani, uweke nywele za namna fulani, utumie manukato fulani.
Ambacho wengi wetu tunasahau sasa ni kwamba, haya makampuni ya kibepari
ya nywele bandia, manukato, nguo, pochi, kucha bandia wanatumia watu
maarufu kuuza bidhaa zao ili sisi wanyonge tuone ndiyo mambo ya kisasa
na kuanza kupapatika nayo mwishowe tunazidi kuwa maskini ilhali wao
wakipata utajiri maradufu.
Huu ni unyonyaji wa hali ya juu, yatupasa kufikiria upya namna ya
maisha yetu na kufanya mambo yenye tija ili kulikomboa taifa letu. Hapa
utasikia watu wakisema sasa tufanyaje na ndiyo hali ya dunia
inavyokwenda yatupasa kwenda na kasi hiyo.
Inatupasa kama taifa kuliona hili ili kuweza kulikomboa kwa kuwa na
mijadala kila mahali nchini kwani ukisema tufanye hivi utapata jibu la
Haki za Binadamu.
Kwa upande mwingine, ili kutengeneza soko zuri kwa mabebari ni sharti
kutengeneza taifa tegemezi ambalo litakuwa siyo bunifu na mwishowe kutoa
masoko ya uhakika.
Sasa hivi Tanzania kama taifa lina vita kubwa ya kupambana dhidi ya
mitandao ya kijamii kwani wengi wetu tumesha athirika kiasi kwamba
ukikaa dakika mbili mbali na simu yako unajihisi mgonjwa. Tumekuwa
walevi wa simu (addicted) kama wenye kutumia madawa ya kulevya au walevi
wa pombe ambao hawaendeshi maisha pasi utumiaji wa vileo.
Kiuhalisia jaribu kukaa na jamaa zako kama wanne mkiwa mahali katika mazungumzo ya jioni
halafu angalia vile watu walivyokuwa karibu na simu zao kiasi kwamba
meza inakosa mazungumzo kabisa. Ingawa mkoa pamoja, lakini kila mmoja
yuko mbali, amezama kwenye simu na wakati mwingine anaweza kununa ama
kuangua kicheko kutegemeana na ujumbe aliousoma kwenye mtandao wa
kijamii.
Siku hizi hata familia nyingi watoto wanakosa uangalizi mzuri kwani
wazazi wakirudi nyumbani nao wako karibu na simu zao kuliko vile walivyo
karibu na watoto wao.
Je, hii siyo aina nyingine ya umaskini? Sehemu muhimu ya maendeleo ya
binadamu ni kuhakikisha watu wanakutana pamoja kujadili maendeleo ya
nchi yao kwa hoja.
Leo sote fikra zetu ziko kwenye kuangalia mitandao ya kijamii na kusahau kufanya mijadala yenye tija kwa taifa letu.
Leo hii kukitokea ajali kila mtu anataka kuwa mwandishi wa habari wa
kwanza kutoa taarifa ya tukio la ajali badala ya kuanza kuwaokoa
majeruhi katika ajali hiyo.
Fikra zetu ndizo mkombozi wetu kwani zinatuletea ubunifu katika maisha
ili kuweza kufanya mambo yenye tija katika taifa ila kwa kuwa
tumeukumbatia ubepari kwa dhati, ubepari huo umeteka fikra zetu kiasi
kwamba tunasahau kubuni mambo ya msingi ya jamii zetu na kubaki kuwa
walaji wa yale yote yanayoletwa na nchi za Magharibi.
Mitandao ya kijamii imefanikiwa kuteka fikra zetu na ubunifu wetu na hivi ndivyo Tanzania itaendelea kuwa maskini.
0 comments:
Post a Comment