Baada ya matukio ya kutisha kutokea mara kwa mara katika mtaa wa Utemini
kata ya Mkolani Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, mwenyekiti wa mtaa
huo, Jukaeli Kiula, ameamua kuzinunulia filimbi kaya 60 kwa lengo la
kujihami na matukio ya kihalifu.
Akiongea na gazeti la Nipashe Ijumaa hii, Mwenyekiti wa mtaa huo,
alisema ameamua kuwanunulia filimbi wananchi wake ili waweze kutoa
taarifa za uhalifu pindi wanapovamiwa.
“Wananchi wangu wameingiwa na hofu kubwa baada ya matukio mawili ya
mashambulizi yaliyotokea…kubwa wanahofu wanaweza kuingiliwa na watu
wasio wema katika nyumba zao,” alisema.
Alisema pamoja na polisi kufanya doria mara chache katika mtaa huo,
lakini kama kiongozi wa wananchi hao ameamua kujitolea kuwanunulia
filimbi za usalama kwa ajili ya kujitetea pale watakapovamiwa na watu
wasiofahika.
Alisema filimbi ni moja ya ulinzi ambao mtu akipiga ni rahisi kufahamu kuna tukio sehemu fulani na kupata msaada wa haraka.
Alisema matukio ya uhalifu na mauaji yaliyotokea kwa kipindi kifupi
ndani ya mwezi mmoja, yalichangiwa kwa kutokuwapo na ulinzi wa
kuaminika, lakini kwa sasa wamejipanga kuimarisha.
Mtaa huo ulikumbwa na majanga likiwamo la mauaji msikiti wa Rahman
Mei 19, mwaka huu, saa 3:00 usiku wakati wa swala ya Isha, baada ya watu
waliokuwa na silaha za kijadi, mapanga na mashoka kuwavamia waumini na
kuwachinja akiwamo imani wa msikiti huo.
0 comments:
Post a Comment