Timu ya taifa ya Misri imekata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon, baada ya kuwafunga wenyeji,
Tanzania mabao 2-0 jioni ya leo uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanawafanya Misri wamalize mechi za Kundi G wakiwa na
pointi 10 baada ya mechi nne, wakishinda tatu na kutoa sare moja, wakati
Tanzania inabaki na pointi yake moja na inashika mkia nyuma ya Nigeria
yenye pointi mbili.
Hadi mapumziko, tayari Misri walikuwa mbele kwa 1-0 bao lililofungwa
na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea ya England, Mohammed Salah dakika
ya 43 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki Mwinyi Hajji Mngwali
kumkwatua nje kidogo ya boksi Nagram Fahmy.
Katika kipindi hicho, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kila upande ulipoteza nafasi za wazi.
Dakika ya 27, mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu
aliunganishia juu ya lango krosi ya Elias Maguri na dakika ya 30,
Nahodha Mbwana Ally Samatta alipewa pasi nzuri na Farid Mussa akapiga
nje.
Kipindi cha pili, Taifa Stars walikianza vizuri na kufanikiwa kupata
penalti dakika ya 53 iliyotolewa baada ya kiungo Himid Mao kuangushwa na
Ame Medhat hata hivyo, mkwaju wa Nahodha Samatta ulipaa juu ya lango la
kipa mkongwe barani, Essam Kamal Tawfik.
Salah akaifungia bao la pili Misri dakika ya 58 baada ya kumpita beki
wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali aliyecheza chini ya kiwango mno hii
leo.
Kocha Charles Boniface Mkwasa akamtoa Mngwali baada ya kuchomesha kwa
mara ya pili na kumuingiza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, aliyekwenda
kumalizia vizuri.
Tanzania; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali/Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’ dk68, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao,
Thomas Ulimwengu/Deus Kaseke dk73, Mwinyi Kazimoto, Elias Maguli/John
Bocco dk62, Mbwana Samatta na Farid Mussa.
Misri; Essam Kamal Tawfik, Alg Gabr Mossad, Ramy Hisham Abdel,
Mohamed Abdel Sayed, Abood Abdulrahamn Amed, Tarek Hamad Hamed, Mohamed
Nasser Elsayed, Mohamem Ahmed Ibrahim/Amr Medhat dk63, Abdallah Mahamoud
Said na Nagram Mohsin Fahmy.
0 comments:
Post a Comment