Tarehe 08.06.2016 majira ya
saa 08:00hrs hadi saa 15:00hrs katika kisiwa cha Maisome kambi ya uvuvi migongo
kata ya Maisome tarafa Kahunda wilaya Sengerema mkoa wa Mwanza,
katika tukio la kwanza askari wakiwa doria katika kisiwa tajwa hapo juu
wakiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Sengerema walifanikiwa
kukamata nyavu (kokolo) haramu za kuvulia samaki 17 na timba 81 ambayo ni
mitego ya kienyeji ya kutegea samaki, vilivyotelekezwa na wavuvi
wasiojulikana baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa askari wanaofanya
doria na misako katika maeneo yao.
Jeshi la polisi linaendelea na
misako pamoja na doria katika kisiwa hicho kwa kuhakikisha watuhumiwa
waliotelekeza nyavu hizo haramu wanakamatwa na wengine wanaoshirikiana nao pia
wanasakwa ili kukomesha uvuvi haramu katika kisiwa hicho, hii ni baada ya
kupokea taarifa kutoka kwa raia wema kwamba katika kisiwa tajwa hapo juu kuna
wavuvi ambao hutumia zana haramu katika shughuli zao za uvuvi za kila siku
kitendo ambacho ni kinyume na sheria na taratibu za nchi.
Aidha tukio lingine sawa na tarehe
na majiara tajwa hapo juu kwenye kisiwa cha Kasarazi kata ya Bulyaheke
tarafa ya Buchosa wilaya ya Sengerema, askari wakiwa doria walifanikiwa
kukamata nyavu haramu za kuvulia samaki 9 na timba 04 zilizotelekezwa na wavuvi
wasiojulikana baada ya kupokea taarifa ya uwepo wa askari wanaofanya
doria katika kisiwa hicho. Jeshi la polisi bado linaendelea na upelelezi pamoja
na msako wa kuwasaka wavuvi wanaojihusisha na uvuvi haramu ili waweze
kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Baada ya zana hizo haramu kukamatwa
ziliteketezwa kwa moto mbele ya uongozi wa kamati ya ulinzi na usalama wa
wilaya na serikali ya vijiji hivyo na wananchi wakishuhudia, huku msako na
doria katika visiwa hivyo na visiwa vingine vya jirani bado unaendelea.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza
kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wananchi
akiwataka waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwani limedhamiria
kukomesha uhalifu katika mkoa wa Mwanza na kusimamia sheria na taratibu za
nchi.
Katika tukio la pili
Mnamo tarehe 08.06.Majira ya saa
13:06 katika kijiji cha Sima kata ya Sima wilaya ya Sengerma mkoa wa Mwanza,
askari wakiwa doria walifanikiwa kumkamata Sophia Sato miaka 54 mkazi wa kijiji
cha Sima akiwa na pombe aina ya gongo lita 64 zikiwa ndani ya nyumba yake
kitendo ambacho ni kinyume na sheria na taratibu za nchi.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa anafanya
biashara hiyo ya kuwauzia wananchi wa kijiji hicho pombe hiyo haramu na
kuifanya kazi hiyo kama chanzo chake cha mapato kitendo ambacho ni
uvunjwaji wa sheria, ndipo jeshi la polisi lilipokea taarifa kutoka kwa raia
wema na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika atafikishwa
mahakamani.
Aidha katika tukio lingine sawa na
tarehe tajwa hapo juu majira ya saa 13:50 katika kijiji hicho cha Sima kilichopo
wilaya ya Sengerema, askari waliokuwa doria walifanikiwa kukamata mitambo
miwili ya kutengeneza pombe haramu ya gongo na mapipa mawili
yaliyotelekezwa na Elizabeth Martine aliyetoroka baada ya kupewa taarifa za
uwepo wa askari wanaofanya doria.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa tajwa hapo
juu amekuwa akijihusisha na utengenezaji wa pombe hiyo haramu kwa muda
sasa, na amekuwa akiwauzia wakazi wa kijiji hicho. Jeshi la polisi linaendelea
na msako wa kumtafuta mtuhumiwa pamoja na kuwasaka wahusika wengine anaoshirikiana
nao katika biashara hiyo haramu ya pombe ya gongo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza
kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wananchi
akiwaomba waendelee kushirikiana na jeshi la polisi ili tujenge sote kwa pamoja
Mwanza salama zaidi na kuweza kukomesha uhalifu katika mkoa wetu.
Imesainiwa na:
Sacp: Ahmed Msangi
Kamanda wa polisi (m) mwanza
0 comments:
Post a Comment