WAKATI Simba ikitarajiwa kukipiga
na Stand United kesho Jumamosi mkoani Shinyanga, mshambuliaji wa Simba, Ibrahim
Ajib, amesema kuwa mechi ngumu iliyobaki kwao ni Yanga kutokana na wachezaji wa
timu zote kukamiana.
Februari 20, mwaka huu, Simba na Yanga zitakutana katika mechi ya raundi ya
pili ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Simba
itakuwa chini ya Kocha Jackson Mayanja ambaye ameiongoza timu hiyo
kushinda mechi sita mfululizo.
Ajib amekuwa katika kiwango cha juu kwa hivi sasa huku akiwa ameshafunga mabao nane katika ligi kuu, hivyo anaweza kuwa mchezaji muhimu katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ajib alisema wanachokiangalia ni ushindi tu katika kila mechi iliyopo mbele yao lakini anaamini mechi yao dhidi Yanga itakuwa ngumu tofauti na watu wanavyofikiria.
“Yanga ni timu nzuri kutokana na aina ya wachezaji wao, imebakia mechi hiyo ambayo naamini itakuwa ngumu sana kwa sababu kila timu itakuwa inahitaji matokeo ya ushindi lakini timu yetu ipo vizuri na hatuwezi kuwahofia kwa sababu malengo yetu ni kushinda kila mchezo.
“Waje tu, kazi itaonekana kati yetu nani anastahili ushindi, ingawa dakika 90 ndizo zitatoa majibu ya kweli, tusubiri tuone itakuwaje,” alisema Ajib.
0 comments:
Post a Comment