Wakati hali ya kisiasa Visiwani Zanzibar ikiwa inazidi kutokota,
bila kujali theluji na baridi kali, Wazanzibari waishio nchini Canada
mnamo tarehe 27 mwezi huu walifanya maandamano katika Mji Mkuu wa nchi
hiyo, Ottawa katika juhudi za kutafuta uingiliaji kati wa kimataifa
katika kusaka suluhisho la amani kwa mgogoro wa kisiasa Visiwani humo.
Wazanzibari hao waliandamana hadi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu wa
Canada kwa lengo la kufikisha ujumbe wao kukhusiana na hali mbaya ya
kisiasa huko Zanzibar.
Akizungumza na Swahilivilla, mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo
Bwana Zamil Rashid alisema kuwa lengo la maandamano hayo ni kuwaunga
mkono ndugu zao Wazanzibari katika harakati za kudai demokrasia ya kweli
na kupinga hatua za kufutwa kwa uchaguzi Mkuu Zanzibar.
“Madhumuni ya maandamano yetu yalikuwa ni kuwaunga mkono ndugu zetu
wa Zanzibar kwa mambo yaliyofanyika, na kwamba hatukubaliani nayo”
alisema Bwana Zamil na kuendelea “Wazanzibari walioko nchini Canada
wanapinga jambo hilo lilofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na matamshi aliyoyatoa Bwana Jecha Salim Jecha ya kufuta uchaguzi”
Aidha maandamano hayo yalikuwa na lengo la kuiomba Serikali ya
Canada kuingilia kati katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa
Visiwani Zanzibar kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Mbali na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Canada, Wazanzibari hao pia
waliandamana hadi kwenye Ofisi za Umoja wa Ulaya nchini humo kwa dhumuni
hilo hilo.
“Vilevile tumefikisha ujumbe wetu kwa Umoja wa Ulaya (EU) ili
walishighulikie swala hili haraka iwezekanavyo kabla hayajatokea maafa
kwa Wazanzibari”, alisema Bwana Zamil.
Katika Risala yao kwa pande zote mbili, waandamanaji hao wametoa
wito wa kutangazwa mshindi badala ya kurejewa kwa uchaguzi kama
ilivyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bwana
Jecha Salim Jecha. “Tumetoa wito wa yule aliyeshinda uchaguzi atangazwe,
na siyo kurejea uchaguzi” alisisitiza Bwana Zamil.
Kwa kufikisha ujumbe wao kwa Umoja wa Ulaya, wazanzibari hao pia
walikuwa na lengo la kutoa wito kwa nchi nyengine duniani kusaidia
katika kuupatia suluhu mzozo wa kisiaza Zanzibar, ikiwemo pia kusitisha
missada ya kiuchumi kwa Tanzania.
“Tumeziomba serikali za Canada, Umoja wa Ulaya na nchi nyengine
duniani kusitisha misaada kwa Zanzibar na Tanzania ili kushinikiza haya
mambo yaliyotokea yasifanyike tena”, alisema Bwana Zamil.
Mbali na Wazanzibari, maandamano hayo pia yalihudhuriwa na
wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Ottawa, Vyuo vyengine, Waandishi wa
Khabari pamoja na wapenda amani na demokrasia duniani.
Kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kinyume na sheria na tangazo la
kurudiwa tena kwa uchaguzi huo kuliwakasirisha Wazanzibari wengi, na
ndiyo moja ya siri ya kujitokeza kwa wingi kwa Wanzibari katika
kufanikisha maandamno hayo.
“Wazanzibari walijitokeza kwa wingi na tumefarajika kwa hilo”,
alisema Bwana Zamil na kuongeza kuwa “Wazanzibari walikasirishwa na
kitendo kile kilichofanywa na Jecha Salim Jecha pamoja na Serikali ya
CCM cha kufuta Uchaguzi na kutaka kurudiwa mwengine”
Alifafanua msingi wa demokrasia umejikita kwenye msemo wa Kiswahili usemao kuwa “asiyekubali kushindwa si mshindani”.
“Maana ya kuwa na mfumo wa vyama vingi ni kukubali kushinda au
kushindwa, sasa ikiwa mmoja kashindwa na hakutaka kukubali kushindwa,
basi itakuwa hakuna haja ya kufanya mambo ya vyama vingi” alifafanua
Bwana Zamil na kusisitiza “Hilo ndilo lililowakasirihswa Wazanzibari,
kwani wanahisi wanadharauliwa”.
Itafaa kukumbusha kuwa mfumo wa vyama vingi ulikuweko Zanzibar
kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964. Kufuatia Mapinduzi hayo mfumo huo
ulitoweka na kurejea tena mwaka 1992 ambapo uchaguzi wa mwanzo
ulifanyika mwaka 1995. Chaguzi zote ambazo hufanyika kila baada ya miaka
mitano visiwani humo huwa zinagubikwa na utata huku Chama Kikuu cha
Upinzani cha Wananchi (CUF) kikidai kuporwa ushindi wake.
Katika sherehe za kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar
zilizofanyika tarehe 12 mwezi huu, baadhi ya wanachama wa Chama Tawala
cha CCM walibeba mabango yaliyokuwa na maneno ya kibaguzi kama vile
kuwataka machotara waondoke na kwamba Zanzibar ni nchi ya Waafrika.
Mabango hayoyalikuwa kama kidonda kipya juu ya kovu mbichi na
kupelekea hali tete zaidi visiwani humo. Kukhusiana na hilo Bwana Zamil
alisema “Eti wanasema machotara wende kwao, haya yote yamewakera
Wazanzibari, kwa sababu, matusi kama yale ni matusi ya kibaguzi”
Mada hiyo pia ilijitokeza kwenye maadamano ya jijini Ottwa ambapo
baadhi ya mabango yalibeba ujumbe uliosomeka “Ubaguzi ni saratani kwa
jamii ya Zanzibar yenye mchanganyiko wa watu wa rangi tofauti, wakati
umefika sasa wa kumaliza ubaguzi wa rangi”
Baadhi ya mabango hayo yaliyoandikwa kwa lugha rasmi za Canada za
Kiengereza na Kifaransa, yalibeba ujumbe ukiitaka serikali ya nchi hiyo
kukata uhusiano wa Kibalzi na Tanzania, kusimamaisha misaada ya kiuchumi
kwa Tanzania na Zanzibar, kupinga kurudiwa kwa uchaguzi na badala yake
kutangazwa mshindi wa Uchaguzi uliopita, kumsuta Rais Magufuli kwa
kujishughulisha na kuzuia ubadhirifu wa fedha za taifa badala ya kuzuia
damu za Wazanzibari zisimwagike na mengineyo.
Akijibu swali la mwandishi wetu iwapo kuna majibu yoyote kwa risala
yao, Bwana Zamil alisema “Wamesema kuwa watalishughulikia haraka
iwezekanavyo kabla mambo hayajaharibika zaidi Zanzibar”.
Aliongeza kuwa Afisa wa Umoja wa Ulaya aliepokea risala yao
aliahidi kuifanyia kazi mara moja. “Amesema leo hii ataisambaza kwa
wanachama wote wa Umoja huo ile risala ili waisome na kuchukua hatua za
haraka zaidi” alisisistiza Bwana Zamil.
Kukhusu ukimya wa Rais wa Tanzania juu ya yale yanayoendelea
Zanzibar, Bwana Zamil amlimtolea wito Dkt John Pombe Magufuli
kuushughulikia mzozo wa Zanzibar ili kuepusha janga la kibinadamu.
“Rais wa Tanzania ana jukumu, ni lazima asimamie haki na usalama wa
Wazanzibari wote, na Wazanzibari lazima haki yao aisimamie, siyo kama
hivi kukaa kimya” alisihi mwanaharakati huyo, na kuongeza, “Hii
inaonesha kama kwamba anakubaliana na yale yanayotokea Zanzibar”
Kwa upande mwengine, mwanaharakati huyo aliwatolea nasaha WanaCCM
wa Zanzibar kwenda na wakati na kuwa washindani wa kweli, huku wakijua
demokrasia ni kubadilishana madraka kwa njia za amani.
“Zanzibar ni mali ya Wazanzibari wote na wala siyo milki ya CCM.
Kwa hiyo aliyeshindwa akubali kushindwa, na aliyeshinda wampongeze ili
watu waishi kwa hali ya mapenzi na amani kuliko kusubiri mpaka watu
kupigana, mambo ambayo yataleta madhara makubwa”, alisema Bwana Zamil na
kuonya “…inaweza kufika mahala watu kufikishana kwenye Mahakama za
Kimataifa”
Alitoa ukumbusho kwa viongozi walioko Madarakani Zanzibar kuwa
kinga ni bora kuliko tiba, na kusema “Ningeiomba Serikali isikubali
kufika huko” Halkadhalika alitoa wasia maalum kwa Rais wa Zanzibar Alhaj
Ali Mohammed Shein kwa kusema “Namuusia Rais Shein asikubali kufikishwa
mahala ambapo patakuja kumletea khasara hapa dunianiu na huko Akhera”
Maandamano ya Wazanzibari nchini Canada yanakuja kufuatia yale ya
Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA) yaliyofanyika
Ikulu ya nchi hiyo (White House), na kwenye Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa jijini New York.
Maandamano kama hayo pia yalifanyika nchini Uingereza na sehemu
nyengine za Ulaya. Kwa muqtadha huu Bwana Zamil amewatolea wito
Wazanzibari popote Ulimwenguni kuchukua hatua za kushinikiza kupatikana
ufumbuzi wa amani kwa mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
“Nawashauri Wazanzibari walioko katika sehemu nyengine duniani
waungane na Wazanzibari wenzao ili kupigania demokrasia ya kweli katika
nchi yao” alishauri, na kunasihi “Na katika kufanya hivyo, wapiganie kwa
njia za amani haki na usawa”
Vile vile, Bwana Zamil alitoa shukrani maalum kwa Polisi wa Canada
kwa ushirikiano wao mzuri tangu mwanzo mpaka mwisho wa shughuli yao.
Ikumbukwe kwamba, mgogoro wa sasa wa kisiasa Zanzibar uliripuka
kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana baada ya
uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Bwana Jecha Salim
Jecha wa kutangaza kuufuta uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake kwa
madai ya kuwepo kwa kasoro nyingi za uchaguzi khususan Kisiwani Pemba
ambako ndiko kwenye ngome kuu ya Chama cha upinzani cha CUF.
Wataalamu wa maswala ya Sheria za Zanzibar wanaona kuwa hatua hiyo
ya Bwana Jecha haikuwa ya kisheria, na wasimamizi wa uchaguzi,
wachunguzi, wadadisi na wachambuzi wa nje na ndani ya nchi waliuelezea
uchaguzi huo kuwa ulifanyika katika mazingira huru na ulikuwa wa haki.
Inaaminika kuwa hatua ya kufutwa kwa uchaguzi huo ilikuja baada ya
kubainika kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha CUF Maalim Seif
Sharif Hamad alikuwa amemtangulia mpizani wake mkubwa aliyekuwa akitetea
kiti chake Rais Ali Mohammed Shein.
Kufuatia kufutwa kwa uchaguzi huo, vikao vya siri vya mzungumzo
vilifanyika kwa zaidi ya miezi miwili katika Ikulu ya Zanzibar
vikiwashirikisha Rais Ali Mohammed Shein, Makamo wake wa Kwanza Maalim
Seif Sharif Hamad, Makamo wa Pili Balozi Seif Ali Idd pamoja na Marais
wastaafu wa Zanzibar, Mabwana Amani Karume, Salmin Amour na Ali Hassan
Mwinyi.
Wakati vikao hivo vya siri vikiwa vinaendelea, mitaani kukazaliwa
msamiati mpya uliojulikana kwa jina la “drips” zikiwa ni tetesi kuhusu
kile kinachoendelea katika mazungumzo hayo.
Hatimaye mfuko wa drips ukapasuliwa baada ya mazungumzo hayo
kushindwa kufikia mwafaka, na Bwana Jecha kujitokeza tena na kutangaza
kuwa uchaguzi utarudiwa tarehe 20 Machi mwaka huu na hivyo kupelekea
mtafaruku zaidi wa kisasa Visiwani humo.
Kufuatia uamuzi huo, chama cha CUF kimesema kuwa hakitoshirki
kwenye uchaguzi wa marudio, na kushikilia msimamo wake wa kutaka matokeo
ya uchaguzi wa Oktoba yatangazwe, kwa vile uchaguzi ulikuwa huru na wa
haki.
Hali ya mgando wa kisiasa Zanzibar imepelekea athari mbaya za
kiuchumi na kijamii, huku mfumko mkubwa wa bei khususan bidhaa muhimu
kama vile chakula ukiarifiwa kufikia zaidi ya asili mia 10.
0 comments:
Post a Comment