Mwanasiasa maarufu na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa ameibuka na
kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.
Dk. Slaa ambaye kwa sasa yuko Canada, amesema kutokana na hali ya
mambo yanayoendelea hivi sasa nchini ni jukumu la Bunge kuhakikisha
utawala wa mabavu unaofanywa na baadhi ya viongozi madarakani
hautokei.
Akizungumza mwanzoni mwa wiki akiwa Canada, Dk. Slaa, alipongeza
uongozi wa Rais Dk. John Magufuli akisema yale aliyokuwa akiyapigia
kelele kwa zaidi ya miaka 10 sasa yanatekelezwa.
“Kwa siku 100 ambazo Rais Magufuli yuko ofisini nadhani kama kuna jambo ninatakiwa kusema ni kumpongeza, kumtakia heri.
“Huko nyuma nilitoa kauli kwenye mtandao kuwa jukumu sasa ni la
Bunge, bila itikadi ya vyama, kumsaidia Rais hayo aliyoyaanza yaweze
kutekelezwa, kuhakikisha kuwa framework (utaratibu) sahihi wa kulinda
haki kwa maana marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu
inapohitajika.
“Pia ni jukumu la Bunge kuhakikisha udikteta unaohofiwa na baadhi ya
watu hautokei. Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ‘ukiachiwa atakuwa
dikteta’. Vyombo vyote vifanye kazi kwa mujibu wa Sheria,”alisema Dk.
Slaa.
Alipoulizwa kuhusu hatima yake katika siasa, alisema tangu
alipoondoka Oktoba mwaka jana kwenda Canada ambako anasoma mambo
mbalimbali alisema;
“Kabla ya kuondoka Tanzania niliwaaga Watanzania kwa programu kadhaa
zilizorushwa live (moja kwa moja). Niliwaaga kuwa naenda ‘sabbatical’,
kwa lugha nyingine nitasoma mambo mbalimbali.
“….nilishawahi kueleza kuwa kwa sasa ninasoma Psychoanalysis na
Psychotherapy (kwa kuzingatia kuwa Major Seminary nilisoma idara zake
zote ikiwa ni pamoja na Psychology). Hivyo bado nasoma ninanoa akili
zangu,” alisema Dk. Slaa.
Akizungumzia kuuzwa kwa nyumba yake iliyopo Mbweni Dar es Salaam
baada ya kushindwa kurejesha mkopo wa benki, alisema yeye na mke wake
hawajawahi kuchukua mkopo wa aina yoyote benki.
“Nataka nikuambie na uwajulishe Watanzania kwamba wala si mimi Dk.
Slaa wala mke wangu, Josephine kwa wakati wowote ule hatujawahi kuchukua
mkopo benki.
“Tangu nimetoka bungeni sijawahi kuchukua hata senti moja benki, achilia mbali propaganda ya Sh milioni 300.
“Hivyo ni vizuri waliokupa taarifa wakupe undani ni benki ipi
nilikopa au Josephine alikopa na ni shilingi ngapi na kwa nyaraka zipi
tulikopa. Ni vema pia ukafuatilia na benki husika kama walikuambia ni
benki gani.
“Na sisi huku tunasikia taarifa ya nyumba yetu kuuzwa. Kwa hatua ya
sasa sidhani kuwa ni suala la kwenye magazeti. Ninachukua hatua stahiki
kwa mujibu wa sheria dhidi ya wote waliohusika,” alisema.
Maoni yake kuhusu hali ya siasa Visiwani Zanzibar hasa baada ya
kufutwa matokeo Oktoba 28, mwaka jana na kutangazwa uchaguzi wa marudio
Machi 20, mwaka huu, alisema kwa vile kipindi chote amekuwa nje ya nchi
hivyo hawezi kuzungumzia kuhusu suala hilo.
“Mambo ya Zanzibar yana sura ya sheria na procedure (utaratibu) ikiwa
ni pamoja na taratibu zilizotumika. Kipindi chote hicho nimekuwa nje.
“Sina tabia ya kukurupikia jambo ambalo sina taarifa kamili nalo.
Taarifa pekee zinazopatikana ni za kwenye mitandao ambayo wewe mwenyewe
ni shahidi kuwa mengi yanawekwa chumvi au hata kutengenezwa kwa sababu
za propaganda.
“Mimi niko nje ya ‘active party politics’ kama nilivyotangaza
Septemba Mosi mwaka jana, hivyo siendekezi propaganda wala mambo
yaliyowekwa chumvi au hata yale ambayo siyafahamu vizuri,” alisema Dk.
Slaa.
Katibu Mkuu huyo wa zamani ya Chadema, alitangaza kujiengua katika
uongozi Septemba Mosi mwaka jana baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kujiunga na chama hicho.
CHANZO MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment