WINGA
chipukizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid
Mussa, aliyeko majaribioni nchini Hispania, jana aliiongoza CD Tenerife
ya Ligi Daraja la Kwanza nchini humo ‘Segunda Division’ kuichapa UD
Diabora bao 1-0.
Habari njema zaidi kuhusu Farid ni winga huyo kufanya vizuri katika
mtihani wake huo wa kwanza baada ya kuwapagawisha viongozi na benchi la
ufundi la Tenerife.
“Naendelea vizuri sana na jana usiku nilicheza dakika 45 katika
mchezo wa kirafiki na nimeiongoza timu hiyo kupata ushindi, nimefanikiwa
kuivutia hii timu kwani walishangazwa na kiwango changu kizuri hadi
kudiriki kuniuliza kama kweli mimi ni Mtanzania baada ya mechi hiyo,”
alisema Farid wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu
Kwa mujibu wa wakala wa Farid, John Sorzano raia wa Venezuela
aliyeishi sana nchini England, amedai kuwa wiki ijayo nyota huyo
anatarajia kuanza rasmi majaribio katika timu mbili za Ligi Kuu Hispania
‘La Liga’ akianzia Las Palmas na kumalizia Malaga.
Farid atafanya majaribio hayo na kukaa huko kwa wiki mbili zijazo
akitarajiwa kurejea nchini Mei 19 mwaka huu wakati msimu huu wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakapokuwa umemalizika.
Lakini mechi pekee ambayo anaweza kuiwahi ni ile ya fainali ya Kombe
la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) itakayofanyika Mei 25 mwaka
huu, ambayo Azam FC ilitinga juzi kwa kuichapa Mwadui ya Shinyanga na
itacheza na mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Yanga na Coastal
Union.
0 comments:
Post a Comment