Ni eneo la Vijibweni na Kurasini wilayani Kigamboni jijini Dar es
Salaam, ndipo utakapolikuta daraja la kisasa linaloning’inia kwa nyaya
mbalimbali ambazo kiitaalamu ndio zinazobeba uzito wa magari na watu
wanaolitumia daraja hilo.
Ukifika eneo hilo, utashuhudia mandhari ya kuvutia ya barabara za
kisasa zilizopambwa na taa za rangi mbalimbali, hasa nyakati za usiku
pamoja na barabara za juu zinazoelekea pande mbalimbali za jiji hilo la
Dar es Salaam.
Daraja la Nyerere ni daraja la kipekee kujengwa nchini
Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, kutokana na ukweli kuwa ni daraja
la kwanza kujengwa baharini lakini pia ni daraja lililojengwa kwa
gharama kubwa kutokana na ujenzi wake kutumia teknolojia ya kisasa zaidi
katika eneo la kuhimili uzito.
Urefu wa daraja hilo lililopewa jina la muasisi wa Tanzania na Baba
wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ni mita 680 na upana wa mita 32,
na lina barabara sita, tatu zikitoka Kigamboni kwenda Kurasini na tatu
kutoka Kurasini kwenda Kigamboni. Aidha daraja hilo lina urefu wa mlazo
wa kilometa mbili na nusu.
Ukweli ni kwamba mtindo wa ujenzi wa daraja hilo ni wa kipekee katika
nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa linakuwa daraja la kwanza
kujengwa kwa mtindo wa kuning’inia ambao kwa lugha ya kitaalamu unaitwa
‘cable stayed bridge’. Kumalizika na kuanza kutumika rasmi kwa daraja
hilo, kunahitimisha usemi maarufu unaosema hakuna marefu yasiyo na nchi
na waswahili husema ‘hayawi hayawi sasa yamekuwa’.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba daraja hilo limekuwa likisubiriwa
kwa hamu na wakazi wa Dar es Salaam hususani wa maeneo ya Kigamboni kwa
muda mrefu.
Historia ya ujenzi wa daraja hilo, inaanzia miaka mingi
iliyopita 1930s ambapo kumekuwepo na mipango na mikakati ya kujenga
daraja hilo ikiwa ni moja ya njia ya kuwarahisishia wakazi wa ‘kisiwa’
hicho cha Kigamboni usafiri wa kufika eneo la katikati ya jiji la Dar es
Salaam.
Pamoja na kwamba ujenzi wa daraja hilo ulionekana kama ndoto
isiyotimia hasa kutokana na ukosefu wa fedha wa Serikali na suala
lenyewe kuchukua muda mrefu, sasa hali imebadilika kwani tayari ujenzi
wake uko katika hatua za mwisho lakini matumizi ya daraja hilo,
yameshafunguliwa rasmi.
Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa Ujenzi wa daraja
hilo la Nyerere, Mhandisi Karim Mattaka kutoka Shirika la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) daraja hilo ni imara na litaweza kudumu na kutumiwa na
watanzania kwa zaidi ya miaka 100.
0 comments:
Post a Comment