Halmashauri ya Jiji la Mwanza,
imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 1 baada ya kupunguza matumizi
yasiyo ya lazima tangu mwezi Januari mwaka huu na kuzielekeza fedha hizo kwenye
utengenezaji madawati 6,840.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Adam
Ngowi, amesema uamuzi wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ulifikiwa ili
kutekeleza agizo la rais Dkt. John Magufuli linalotaka ifikapo Juni 30 mwaka
huu tatizo la madawati liwe limemalizika.
Ngowi amesema wanafanya utengenezaji
wa madawati hayo ili kupunguza pengo la madawati 11,400 ambalo linasababisha
wanafunzi zaidi ya elfu thelathini kujifunza wakiwa wamekaa chini katika
halmashauri hiyo.
Aidha, amesema kuwa katika utatuzi
wa changamoto hiyo wanakumbwa na changamoto ya upatikanaji wa vifaa ikiwemo
mbao hali ambayo inafanya utengenezaji wa madawati hayo kwenda taratibu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya
Nyamagana, Baraka Konisaga ametembelea kuona hali halisi ya utengenezaji wa
madawati hayo na kusema kuwa kutokana na changamto hiyo wanaweza kufanikiwa
kutatua tatizo hilo lakini sio kwa muda ambao wamepangiwa.
Konisaga amewataka wakazi wa wilaya
ya Nyamagana kila mmoja wao kwa nafasi yake achangie jitihada hizo za
kukamilisha madawati ili kuendana na muda uliopangwa na rais kukamilisha zoezi
hilo.
0 comments:
Post a Comment