728x90 AdSpace

  • Latest News

    Friday, February 12, 2016

    MAAMUZI RASMI YA BASATA KUHUSU "SHIKA ADABU YAKO" YA NAY WA MITEGO TAYARI YAKO HAPA.

    Sasa ni rasmi wimbo wa rapa Ney wa Mitego ‘shika adabu yako’, umefungiwa na Baraza la sanaa Tanzania BASATA.




    Taarifa rasmi kutoka BASATA inasema kuwa mbali na kuufungia wimbo huo, itatoa onyo kali kwa msanii huyo kuacha kutoa nyimbo zenye maudhui ya kuudhi na kinyume cha maadili.
    BASATA pia limemtaka msanii huyo kuacha kuiongelea ‘ngoma’ hiyo katika vyombo vya habari kwa namna yoyote ile

    Usome waraka mzima wa BASATA na maamuzi yao hapo chini,
    Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 4 (1) (j) cha sheria ya BASATA
    namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepwa mamlaka ya kuratibu na kufuatilia
    mienendo ya mtu yeyote anayehusika na kazi za Sanaa na kuhakikisha
    linalinda maadili ya kitaifa miongoni mwa Wasanii wanapokuwa jukwaani au
    wanapobuni kazi yoyote ya Sanaa.


    Aidha, kifungu cha 4 (2) cha sheria hii kinalipa Baraza nguvu ya
    kisheria kufanya jambo lolote lile kuliwezesha kufanya majukumu yake kwa
    faida na ustawi wataifa.


    Baraza la Sanaa la Taifa limekuwa likipokea simu za maswali na
    malalamiko kadhaa kutoka kwa waandishi wa habari na wadau wa Sanaa ambao
    kwa njia moja ama nyingine wameguswa na kuchukizwa na kazi hiyo ambayo
    si tu inadhalilisha tasnia ya Sanaa bali inawafanya watu makini kuanza
    kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya Sanaa kwa ujumla.


    BASATA mara kadhaa limekuwa likikemea na kuchukua hatua kadhaa dhidi ya
    tabia hii chafu ambayo ilianza kujitokeza kwenye kampeni za uchaguzi
    mkuu wa mwaka jana wa 2015. Kukemea huku ni kwa msingi mmoja kwamba
    asili ya tasnia hii ya Sanaa ni kuelimisha jamii, kukosoa pale
    kunapokuwa na tatizo, kuburudisha na kujenga jamii yenye staha, umoja wa
    kitaifa, mshikamano na amani.


    Ni wazi wasanii wengi wanafanya kazi zao vizuri, kwa kubuni kazi zenye
    ubora, zenye kujenga jamii na zaidi zinazoburudisha rika zote kiasi cha
    kuzifanya zililetee heshima taifa. Kati ya hawa wengi, kuna wachache
    ambao wanaipaka matope tasnia ya Sanaa na kwa kiasi kikubwa wanaonesha
    wazi kutokuwa na nia njema.


    Kwa mantiki hii BASATA halitavumilia hawa ‘wasanii’ wachache ambao
    wanataka kuigeuza tasnia ya Sanaa na wasanii genge la wahuni, wasio na
    staha, wa kudharaulika na waliojipanga kuibomoa jamii na kuharibu amani
    na utulivu uliopo nchini.


    BASATA linapenda kueleza yafuatayo:
    1. Vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya
    Sanaa kabla ya kuingia kwenye mtego wa kuwa mawakala wa uharibifu wa
    jamii kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa. BASATA lilishaziandikia radio
    zote kuzishauri kuwa na kamati za maudhui ya kazi za Sanaa lakini
    inashangaza baadhi ya vyombo vya habari vinakuwa vya kwanza kushabikia
    nyimbo hizo chafu na kuwapa muda mrefu wa mahojiano wasanii hao na
    baadaye kurudi BASATA kuhoji uhalali wa nyimbo husika. Hii si sawa hata
    kidogo.


    2. Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli
    imejipanga kuwajengea mazingira bora ya utendaji Wasanii wote nchini
    kupitia kuboresha miundombinu ya Sera, Sheria na Kanuni. Hata hivyo,
    uwepo wa Wasanii kama hawa unafanya jamii kuhoji hadhi ya wasanii,
    nafasi yao katika jamii na kwa maana hiyo kukatisha tamaa juhudi za
    kuipa msukumo sekta hii maana wadau wakuu ambao ni wasanii wanaanza
    kuoneasha kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii.


    3. BASATA linawataka wasanii kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi
    zao za Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao
    watazipokeaje? Wavae nafasi ya wale wanaowatukana na kuwadhalilisha,
    Waelewe kwamba Sanaa si uwanja wa kutusi na kudhalilisha watu hata
    kidogo. Ikitokea wale wanaotukanwa na kudhalilishwa kughafilika Sanaa
    itakuwa uwanja wa vita. Hili halikubaliki.


    4. Tunafahamu kuna wasanii wamekuwa wakifanya hivyo makusudi kutafuta
    ‘umaarufu uchwara’ ambao wanadhani utakuja kutokana na kuzungumziwa
    sana. Tunapenda kusema wazi kwamba umaarufu hauji kwa upuuzi wa namna
    hiyo unakuja kwa msanii mwenyewe kujiheshimu, kujituma, kubuni kazi bora
    na zenye kulifahamu vema soko la ndani na la kimataifa.


    SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
    Godfrey L. Mngereza
    KATIBU MTENDAJI, BASATA
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: MAAMUZI RASMI YA BASATA KUHUSU "SHIKA ADABU YAKO" YA NAY WA MITEGO TAYARI YAKO HAPA. Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top