HABARI LEO.
WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema mgombea urais wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa anasahau haraka na
kuanza kunadi miradi ambayo imeshaanza kujengwa na Rais Jakaya Kikwete
kupitia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akitoa mfano, Sitta alisema anamshangaa Lowassa kusema atajenga Reli
ya Kati akichaguliwa kuwa rais wakati mradi huo ulishaanza maandalizi
yake na sasa utawekewa jiwe la msingi na Rais Kikwete Septemba 15, mwaka
huu, hafla itakayofanyika eneo la Soga Mpiji wilayani Bagamoyo mkoani
Pwani.
Aidha, amesema wananchi hawawezi kukaa kimya bila kuhoji suala la
kashfa ya Richmond, kama alivyodai Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
kwa sababu tu baada ya Lowassa kujiuzulu, kuna ufisadi mwingine
ulitokea.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sitta alisema
mbali ya mradi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, ujenzi
wa reli nyingine ya Kusini kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay mkoani
Ruvuma, utaanza kabla Rais Kikwete hajaondoka madarakani.
“Sijui hawa wenzetu waliotoka CCM sijui wana matatizo ya kusahau…
wanataja miradi ambayo Rais Kikwete anaitekeleza. Lowassa anataka
kujenga Reli ya Kati ipi? Yaani mgombea urais amesahau kuwa reli hii
inajengwa na JK?” alihoji Sitta.
Kuhusu mradi huo, alisema baada ya Rais kuweka jiwe na msingi, ujenzi
wa reli hiyo utafanywa na Kampuni ya China Railway Construction kwa
miaka minne na nusu kwa gharama ya Sh trilioni 16.
“Hii kampuni ilikuwa inajenga reli kama hiyo ya kiwango cha juu, kati
ya Addis Ababa hadi Djibouti, sasa wamemaliza ujenzi na Septemba 9,
mwaka huu, baadhi ya vifaa vya ujenzi vitawasili nchini na nitavipokea
pale bandarini,” alisema Sitta.
Alisema mipango ya ujenzi wa reli hiyo haijaanza sasa, kwani
ilikuwepo kwa miaka mingi nyuma chini ya Waziri Dk Harrison Mwakyembe,
na kuongeza kuwa mpango ni kujenga reli ya kisasa itakayowezesha treni
kusafiri kwa kilometa 120 kwa saa na kubeba tani milioni 25 kwa mwaka.
“Kiwango hiki cha bidhaa si kidogo ni kikubwa sana na hapa ndipo
linapokuja wazo la kujenga Bandari ya Bagamoyo kwani Bandari ya Dar es
Salaam itazidiwa sana maana nchi nyingi zitapitisha mizigo yao nchini
kutokana na urahisi wa kusafirisha mizigo kwa njia ya reli ya kati,”
alisema.
Kuhusu Reli ya Kusini, alisema ujenzi wa reli hiyo ya kisasa pia
utaanza kabla ya Rais Kikwete kuondoka madarakani na itaanzia Mtwara
hadi katika Bandari ya Mbamba Bay ili kusafirisha rasilimali za chuma,
makaa ya mawe na gesi, akisema hatua hiyo itakuza uchumi wa wananchi wa
kusini ndani ya miaka minne ijayo.
Akizungumzia kuhusu kashfa ya Richmond iliyomfanya Lowassa ajiuzulu
nafasi ya Uwaziri Mkuu Februari 2008, Sitta alisema si sawa kwamba
wananchi wasihoji kashfa hiyo kwa vile baada ya Lowassa kuondoka
madarakani, ufisadi mwingine ulitokea.
Alikuwa akijibu hoja ya Sumaye kwamba kwa nini suala la Richmond
linahojiwa wakati zipo kashfa nyingine nyingi, ziliibuka baada ya
Lowassa kujiuzulu, akizitaja za mabehewa mabovu, kusafirishwa kwa twiga
kwenda nje ya nchi, kuchotwa kwa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow
na nyinginezo.
“Hili ni jambo la ajabu, ni lazima watu wahoji suala la Richmond kama
ambavyo ni lazima wahoji kashfa nyingine zilizotokea. Suala la Richmond
lilishughulikiwa kama lilivyoshughulikiwa na kashfa nyingine
zilizoibuka pia zilishughulikiwa kwa namna yake na hayo yote ni lazima
yahojiwe na wananchi,” alisema Sitta ambaye wakati Lowassa anaachia
ngazi bungeni mwaka huo, alikuwa Spika wa Bunge.
Kuhusu Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), alisema serikali inaendelea
kuchanganua madeni ili kusafisha mizania yake kwa lengo la kukopesheka
na kwamba wanakusudia kununua ndege nne ifikapo Desemba mwaka huu.
MTANZANIA
MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
Edward Lowassa, amewataka Watanzania wasiogope kufanya mabadiliko ya uongozi
kwa kuwa hata Biblia inasisitiza watu wasiogope.
Amesema ili mabadiliko hayo yafanikiwe,
Watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi Oktoba 25, mwaka huu na kumpigia
kura za ndiyo pamoja na wagombea ubunge na udiwani kupitia Ukawa.
Lowassa aliyasema hayo jana katika mji wa
Makambako, mkoani Njombe alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa Jimbo la
Makambako.
“Jamani wananchi wa Makambako, nawaambia nataka
kura za kutosha kuniingiza Ikulu, nikiingia madarakani nchi itakuwa tulivu na
hakuna atakayemwaga damu.
“Tukichukua nchi hii itakuwa tulivu, hatutaki
kumwaga damu na kama ni damu kumwagika, watamwaga wao na wala siyo sisi.
“Kwahiyo, nasema ‘I am serious’, nataka kura za
kutosha kwa sababu naambiwa wale wenzetu (CCM) ni mabingwa wa kuiba kura.
Nataka watakapoiba, zibaki nyingine za kutuwezesha kushinda.
“Hata nyie mnaotaka kuhama hameni wala msiogope
kufanya mabadiliko kwa sababu neno usiogope limeandikwa mara 365 katika Biblia…
nawaambia msiogope kwa sababu hata mimi siogopi,” alisema Lowassa na
kushangiliwa.
Akizungumzia baadhi ya kero zinazowakwaza
Watanzania, Lowassa alisema kama atafanikiwa kuingia madarakani, Serikali yake
itakuwa makini, kwa kuondoa michango yote ya elimu ya sekondari ili wazazi
wapate nafasi ya kusomesha watoto wao.
“Kuna kero nyingi sana nimeambiwa ziko hapa
Makambako, ambazo naamini ninaweza kuziondoa pindi tu nitakapoingia madarakani.
“Kwanza kabisa, nitaondoa kero ya maji iliyoko
hapa Makambako kwa sababu najua namna ya kuitatua kwa kuwa nilikuwa Waziri wa
Maji enzi za utawala wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
“Pili, hili tatizo la mashine za kukusanya kodi
za EFD nitaliangalia kwa kina kwa sababu haiwezekani nchi ikawa ya kibabekibabe
tu, yaani wafanyabiashara wanasema hivi na wewe hutaki kuwasikiliza.
“Chuo cha VETA kitajengwa hapa Makambako ili
kiwasaidie vijana, matatizo yote ya walimu na wafanyakazi wote serikalini,
nitayatatua kwa sababu uwezo ninao.
“Nitafuta pia michango yote shule za sekondari
kwa sababu chini ya Serikali yangu, elimu itatolewa bure kwani haya yote yako
kwenye ilani ya chama chetu.
“Kwa maana hiyo, nawaomba tena, ikifika Oktoba
25, mwaka huu, mjitokeze kwa wingi kunipigia kura mimi, wabunge wa Ukawa na
madiwani wetu wote ili nikaunde Serikali yenye nguvu,” alisema.
Katika maelezo yake, Lowassa ambaye ni Waziri
Mkuu wa zamani, alisema suala la umasikini kwa Watanzania ni la kujitakia kwa
kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi zinazoweza kuchangia kukuza uchumi wa
Taifa.
Alizitaja baadhi ya rasilimali hizo ambazo
alisema atazitumia kukuza uchumi, kuwa ni pamoja na dhababu, gesi na mazao kama
chai na pamba.
“Kama Mwenyezi Mungu akinijalia, nitaendesha nchi
hii kwa spidi ya ajabu, kwani hatuna sababu ya kuwa masikini.
“Nawahakikishia uchumi wa nchi hii utakua kwa
kasi kwa sababu rasilimali zipo na kinachotufanya tuwe masikini ni kutojua
vipaumbele vyetu,” alisema.
Juu ya migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na
wafugaji, Lowassa alisema itatoweka kwa sababu haiingii akilini Watanzania
waendelee kugombana katika nchi yao, na kwamba ardhi yote itapimwa na wananchi
kumilikishwa ili waitumie kuinua maisha yao.
Baada ya kuhutubia mkutano huo, Lowassa
alihutubia mkutano mwingine mkubwa wa hadhara katika mji wa Njombe na kuwaombea
kura wabunge na madiwani wa Ukawa, huku akisisitiza wananchi wasiichague CCM.
SUMAYE
Awali akihutubia maelfu ya wananchi hao, Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema katika Serikali ya CCM hakuna waziri
anayefaa kupewa madaraka kwa kuwa wameshindwa kuwaletea maendeleo Watanzania.
“Katika Serikali ya CCM, hakuna waziri hata mmoja
mwenye sifa za kupewa madaraka kwa sababu wameiharibu nchi hii. Hakuna hata
mmoja na ndiyo maana namshangaa sana Magufuli (mgombea urais wa CCM) anaposema akiingia
madarakani, atakomesha rushwa wakati na yeye yuko kwenye Serikali iliyojaa
rushwa.
“CCM ni shidaaa, nawaomba msiwape kura kwa sababu
hawana tena uwezo wa kuboresha maisha yenu,” alisema Sumaye.
Katika maelezo yake, Sumaye alionyesha
kushangazwa na baadhi ya maeneo nchini kukosa maji, ukiwamo mji wa Makambako.
“CCM sasa imeanza kusambaza nguzo za umeme katika
maeneo yasiyokuwa na umeme ili wawadanganye wanawaletea umeme, lakini msiwape
kura,” alisema.
Ili kuthibitisha jinsi CCM walivyopoteza mwelekeo,
alimtolea mfano Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Abdulrahman Kinana ambaye
amekuwa akisema baraza la mawaziri lina mawaziri mizigo.
Kutokana na hali hiyo, alisema kama angekuwa
Kinana angelazimika kuihama CCM na kujiunga na Ukawa kwa kuwa ndio wenye nia ya
dhati ya kuwaletea maendeleo Watanzania.
MGOMBEA UBUNGE
Naye mgombea ubunge katika Jimbo la Makambako,
Mhema Oraph (Chadema), aliwaambia wananchi kwamba atakapoingia madarakani,
atatatua kero ya maji, atafuta ushuru usiokuwa na maana, atasaidia upatikanaji
wa umeme na pia atatatua migogoro ya ardhi iliyokithiri jimboni humo.
Wakati huo huo, aliyekuwa Katibu wa Uchumi na
Fedha wa CCM, Mkoa wa Njombe, Ally Mwimike, alitangaza kukihama chama hicho na
kujiunga na Ukawa.
Ingawa hakutaja chama alichojiunga nacho katika
umoja huo, Mwimike alisema Watanzania wanatakiwa kufanya mabadiliko kwa kuwa
CCM imetawaliwa na rushwa.
MWANAHALISI
MGOGORO mpya umeibuka Ngorongoro baada ya Askari wa Wanyamapori wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kudaiwa kuwapiga wafugaji wa kata za
Endulen na Alaitole wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hiyo.
Vurugu hizo zimeibuka mwishoni mwa wiki iliyopita
na kusababisha wafugaji 27 kujeruhiwa huku wengine 22 kuwekwa
kizuizini, pamoja upotevu wa mifugo 52 ambayo haijulikani ilipo.
Chanzo cha mgogoro huo kinaelezwa kusababishwa na baadhi ya wafugaji
kupeleka mifugo yao eneo la Mash ambalo hutumiwa kunywesha mifugo yao
hasa kipindi cha kiangazi, ambapo askari walipowakuta walianza
kuwashambulia kwa madai kuwa hawaruhusiwi kufuga mifugo yao katika eneo
hilo.
Wafugaji hao wameeleza kuwa katika kipindi hiki cha kiangazi ambacho
wanakabiliwa na uhaba wa maji hasa kwa ajili ya mifugo yao na wamekuwa
na utaratibu wa kutumia eneo hilo kwa makubaliano ya kila mwaka ila kwa
mwaka huu imekua tofauti kwani wamefukuzwa pamoja na kupigwa na askari
hao kinyume cha sheria.
Mzee wa mila jamii ya Wamasai, Kadogo Olduati amesema kuwa kwa
kipindi kirefu wameishi katika ardhi mseto yenye mchanganyiko wa
wanyamapori na mifugo pamoja na binadamu bila kusababisha athari zozote
katika kwa mazingira na wanyama.
Olduati ameitaka Mamlaka ya Ngorongoro isiegemee upande wa
wanyamapori na kuwasahau wafugaji ambao hutegemea ufugaji kuendesha
maisha yao ya kila siku.
Katibu wa Baraza la Wafugaji, James Moringe ameiomba mamlaka ya
Ngorongoro na Baraza la wafugaji kwa pamoja kuitisha kikao cha haraka
ili kuepusha mgogoro huo ambao unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na
kuathiri uhifadhi na utalii kwa ujumla.
Mhifadhi wa Ngorongoro hakuweza kupatikana kuzungumzia tikio hilo kwa
kuwa simu yake ya mkononi haikupatikana, lakini pia walinzi waliwazuia
waandishi kuingia ofisini kwake mpaka watakapopata kibali maalum.
NIPASHE.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imepitisha rufaa 13 zilizokuwa
zimewekewa pingamizi za kugombea ubunge katika baadhi ya majimbo nchini
yakiwamo ya Ludewa la Deo Filikunjombe (pichani kushoto), mkoani Njombe
na Bumbuli mkoani Tanga linalotetewa na Januari Makamba.
Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam Ofisa wa Tume,
Athumani Masesa, alisema uamuzi huo umetolewa baada ya kusikiliza rufaa
40 kati ya 56 zilizowekewa pingamizi. Makamba na Filikunjombe ni
miongoni mwa wagombea waliotarajiwa kupita bila kupingwa baada ya
kuwawekea pingamizi wapinzani wao, hasa kutoka vyama vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Alisema tume hiyo ilitulipia mbali pingamizi nyingine 27 baada ya
kupitia maelezo na kubaini kuwa hazikuwa na hoja za msingi za
kuishawishi .
Aliyataja majimbo mengine kuwa ni Bumbuli ambalo mgombea wake wa
CCM, January Makamba, Peramiho la mgombea wa chama hicho, Jenister
Mhagama na Ludewa la Deo Filikunjombe.
Alisema Nec leo inatarajia kuendelea kupitia rufaa nyingine
zilizobakia na baada ya kukamilisha kazi hiyo, wataanza kupitia 196 za
madiwani kwa ajili ya maamuzi.
Awali waliotangazwa kupita bila kupingwa ni Makamba, Rashid Shangazi, Abdallah Chikota(Nanyamba) na Filikunjombe.
0 comments:
Post a Comment