Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan
Ibrahimovic amewahakikishia waandishi wa habari kuwa na furaha ya
kuendelea kuitumikia klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint Germain
licha ya kuelezwa wazi anaweza kusaka mahala pengine pa kucheza soka
lake msimu ujao wa ligi.
Zlatan aliwaeleza waandishi wa habari maneno hayo akiwa kwenye kambi
ya timu ya taifa lake ambayo inajiandaa na michezo ya kuwania kufuzu
kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya dhidi ya Urusi pamoja na
Austria.
Mshambuliaji huyo mwenye kaliba ya kusaka mafanikio kila anapokwenda,
amesema haikuwa mshangao kwake alipowambia anaweza kuondoka kwenye klabu
ya PSG kutokana na kufahamu wazi maisha ya soka namna yalivyo.
Amesema suala la kuhitajika kwenye klabu ya AC Milan ya nchini Italia
ambayo aliwahi kuitumikia kabla ya kuelekea nchini Ufaransa kujiunga na
PSG alilipokea kwa furaha na kukwama kwa mpango huo baada ya dirisha la
usajili kufungwa hakujamuumiza zaidi ya kuangalia namna gani anaweza
kuisaidia PSG ili itetee ubingwa wake msimu huu.
Zlatan amesisitiza kuwa ana mahusiano mazuri na viongozi wa PSG na
kuambiwa wazi jambo la kupewa uhuru wa kuondoka klabuni hapo
haikumaanisha kama palikua na ugomvi ambao ulisababisha kauli hiyo
kutolewa na walio juu yake.
Hata hivyo amedai kwamba kutokana na umri wake kwa sasa anajua
changamoto ua kupambana na vijana wanaoendelea kuchipukia duniani pamoja
na kwenye klabu ya PSG huenda ukawa kikwazo japo anaamini bado ana
uwezo mkubwa wa kupambana.
Zlatan kwa sasa ana umri wa miaka 33 na tayari uongozi wa PSG
umeshaonyesha dhamira ya kupangua safu yake ya ushambuliaji kwa kutaka
kuwasajili wachezaji wengine itakapofika kipindi cha majira ya baridi
(mwezi Januari/ dirisha dogo).
Mbali na klabu ya AC Milan kutajwa kuwa na mkakati wa kumsajili
Zlatan, pia klabu za Arsenal pamoja na Fenerbahce na Galatasaray zote za
nchini Uturuki zinatajwa kuwa na mpango wa kuwania saini ya ibrahimovic.
0 comments:
Post a Comment