728x90 AdSpace

  • Latest News

    Tuesday, September 1, 2015

    NIMEKUWEKEA HABARI KUU KATIKA MAGAZETI MBALIMBALI LEO SOMA HAPA.


    HABARI LEO.
    WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa anasahau haraka na kuanza kunadi miradi ambayo imeshaanza kujengwa na Rais Jakaya Kikwete kupitia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
    Akitoa mfano, Sitta alisema anamshangaa Lowassa kusema atajenga Reli ya Kati akichaguliwa kuwa rais wakati mradi huo ulishaanza maandalizi yake na sasa utawekewa jiwe la msingi na Rais Kikwete Septemba 15, mwaka huu, hafla itakayofanyika eneo la Soga Mpiji wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
    Aidha, amesema wananchi hawawezi kukaa kimya bila kuhoji suala la kashfa ya Richmond, kama alivyodai Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kwa sababu tu baada ya Lowassa kujiuzulu, kuna ufisadi mwingine ulitokea.
    Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sitta alisema mbali ya mradi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, ujenzi wa reli nyingine ya Kusini kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay mkoani Ruvuma, utaanza kabla Rais Kikwete hajaondoka madarakani.
    “Sijui hawa wenzetu waliotoka CCM sijui wana matatizo ya kusahau… wanataja miradi ambayo Rais Kikwete anaitekeleza. Lowassa anataka kujenga Reli ya Kati ipi? Yaani mgombea urais amesahau kuwa reli hii inajengwa na JK?” alihoji Sitta.
    Kuhusu mradi huo, alisema baada ya Rais kuweka jiwe na msingi, ujenzi wa reli hiyo utafanywa na Kampuni ya China Railway Construction kwa miaka minne na nusu kwa gharama ya Sh trilioni 16.
    “Hii kampuni ilikuwa inajenga reli kama hiyo ya kiwango cha juu, kati ya Addis Ababa hadi Djibouti, sasa wamemaliza ujenzi na Septemba 9, mwaka huu, baadhi ya vifaa vya ujenzi vitawasili nchini na nitavipokea pale bandarini,” alisema Sitta.
    Alisema mipango ya ujenzi wa reli hiyo haijaanza sasa, kwani ilikuwepo kwa miaka mingi nyuma chini ya Waziri Dk Harrison Mwakyembe, na kuongeza kuwa mpango ni kujenga reli ya kisasa itakayowezesha treni kusafiri kwa kilometa 120 kwa saa na kubeba tani milioni 25 kwa mwaka.
    “Kiwango hiki cha bidhaa si kidogo ni kikubwa sana na hapa ndipo linapokuja wazo la kujenga Bandari ya Bagamoyo kwani Bandari ya Dar es Salaam itazidiwa sana maana nchi nyingi zitapitisha mizigo yao nchini kutokana na urahisi wa kusafirisha mizigo kwa njia ya reli ya kati,” alisema.
    Kuhusu Reli ya Kusini, alisema ujenzi wa reli hiyo ya kisasa pia utaanza kabla ya Rais Kikwete kuondoka madarakani na itaanzia Mtwara hadi katika Bandari ya Mbamba Bay ili kusafirisha rasilimali za chuma, makaa ya mawe na gesi, akisema hatua hiyo itakuza uchumi wa wananchi wa kusini ndani ya miaka minne ijayo.
    Akizungumzia kuhusu kashfa ya Richmond iliyomfanya Lowassa ajiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu Februari 2008, Sitta alisema si sawa kwamba wananchi wasihoji kashfa hiyo kwa vile baada ya Lowassa kuondoka madarakani, ufisadi mwingine ulitokea.
    Alikuwa akijibu hoja ya Sumaye kwamba kwa nini suala la Richmond linahojiwa wakati zipo kashfa nyingine nyingi, ziliibuka baada ya Lowassa kujiuzulu, akizitaja za mabehewa mabovu, kusafirishwa kwa twiga kwenda nje ya nchi, kuchotwa kwa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na nyinginezo.
    “Hili ni jambo la ajabu, ni lazima watu wahoji suala la Richmond kama ambavyo ni lazima wahoji kashfa nyingine zilizotokea. Suala la Richmond lilishughulikiwa kama lilivyoshughulikiwa na kashfa nyingine zilizoibuka pia zilishughulikiwa kwa namna yake na hayo yote ni lazima yahojiwe na wananchi,” alisema Sitta ambaye wakati Lowassa anaachia ngazi bungeni mwaka huo, alikuwa Spika wa Bunge.
    Kuhusu Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), alisema serikali inaendelea kuchanganua madeni ili kusafisha mizania yake kwa lengo la kukopesheka na kwamba wanakusudia kununua ndege nne ifikapo Desemba mwaka huu.


    MTANZANIA

    MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka Watanzania wasiogope kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuwa hata Biblia inasisitiza watu wasiogope.
    Amesema ili mabadiliko hayo yafanikiwe, Watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi Oktoba 25, mwaka huu na kumpigia kura za ndiyo pamoja na wagombea ubunge na udiwani kupitia Ukawa.
    Lowassa aliyasema hayo jana katika mji wa Makambako, mkoani Njombe alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa Jimbo la Makambako.
    “Jamani wananchi wa Makambako, nawaambia nataka kura za kutosha kuniingiza Ikulu, nikiingia madarakani nchi itakuwa tulivu na hakuna atakayemwaga damu.
    “Tukichukua nchi hii itakuwa tulivu, hatutaki kumwaga damu na kama ni damu kumwagika, watamwaga wao na wala siyo sisi.
    “Kwahiyo, nasema ‘I am serious’, nataka kura za kutosha kwa sababu naambiwa wale wenzetu (CCM) ni mabingwa wa kuiba kura. Nataka watakapoiba, zibaki nyingine za kutuwezesha kushinda.
    “Hata nyie mnaotaka kuhama hameni wala msiogope kufanya mabadiliko kwa sababu neno usiogope limeandikwa mara 365 katika Biblia… nawaambia msiogope kwa sababu hata mimi siogopi,” alisema Lowassa na kushangiliwa.
    Akizungumzia baadhi ya kero zinazowakwaza Watanzania, Lowassa alisema kama atafanikiwa kuingia madarakani, Serikali yake itakuwa makini, kwa kuondoa michango yote ya elimu ya sekondari ili wazazi wapate nafasi ya kusomesha watoto wao.
    “Kuna kero nyingi sana nimeambiwa ziko hapa Makambako, ambazo naamini ninaweza kuziondoa pindi tu nitakapoingia madarakani.
    “Kwanza kabisa, nitaondoa kero ya maji iliyoko hapa Makambako kwa sababu najua namna ya kuitatua kwa kuwa nilikuwa Waziri wa Maji enzi za utawala wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
    “Pili, hili tatizo la mashine za kukusanya kodi za EFD nitaliangalia kwa kina kwa sababu haiwezekani nchi ikawa ya kibabekibabe tu, yaani wafanyabiashara wanasema hivi na wewe hutaki kuwasikiliza.
    “Chuo cha VETA kitajengwa hapa Makambako ili kiwasaidie vijana, matatizo yote ya walimu na wafanyakazi wote serikalini, nitayatatua kwa sababu uwezo ninao.
    “Nitafuta pia michango yote shule za sekondari kwa sababu chini ya Serikali yangu, elimu itatolewa bure kwani haya yote yako kwenye ilani ya chama chetu.
    “Kwa maana hiyo, nawaomba tena, ikifika Oktoba 25, mwaka huu, mjitokeze kwa wingi kunipigia kura mimi, wabunge wa Ukawa na madiwani wetu wote ili nikaunde Serikali yenye nguvu,” alisema.
    Katika maelezo yake, Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani, alisema suala la umasikini kwa Watanzania ni la kujitakia kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi zinazoweza kuchangia kukuza uchumi wa Taifa.
    Alizitaja baadhi ya rasilimali hizo ambazo alisema atazitumia kukuza uchumi, kuwa ni pamoja na dhababu, gesi na mazao kama chai na pamba.
    “Kama Mwenyezi Mungu akinijalia, nitaendesha nchi hii kwa spidi ya ajabu, kwani hatuna sababu ya kuwa masikini.
    “Nawahakikishia uchumi wa nchi hii utakua kwa kasi kwa sababu rasilimali zipo na kinachotufanya tuwe masikini ni kutojua vipaumbele vyetu,” alisema.
    Juu ya migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji, Lowassa alisema itatoweka kwa sababu haiingii akilini Watanzania waendelee kugombana katika nchi yao, na kwamba ardhi yote itapimwa na wananchi kumilikishwa ili waitumie kuinua maisha yao.
    Baada ya kuhutubia mkutano huo, Lowassa alihutubia mkutano mwingine mkubwa wa hadhara katika mji wa Njombe na kuwaombea kura wabunge na madiwani wa Ukawa, huku akisisitiza wananchi wasiichague CCM.

    SUMAYE
    Awali akihutubia maelfu ya wananchi hao, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema katika Serikali ya CCM hakuna waziri anayefaa kupewa madaraka kwa kuwa wameshindwa kuwaletea maendeleo Watanzania.
    “Katika Serikali ya CCM, hakuna waziri hata mmoja mwenye sifa za kupewa madaraka kwa sababu wameiharibu nchi hii. Hakuna hata mmoja na ndiyo maana namshangaa sana Magufuli (mgombea urais wa CCM) anaposema akiingia madarakani, atakomesha rushwa wakati na yeye yuko kwenye Serikali iliyojaa rushwa.
    “CCM ni shidaaa, nawaomba msiwape kura kwa sababu hawana tena uwezo wa kuboresha maisha yenu,” alisema Sumaye.
    Katika maelezo yake, Sumaye alionyesha kushangazwa na baadhi ya maeneo nchini kukosa maji, ukiwamo mji wa Makambako.
    “CCM sasa imeanza kusambaza nguzo za umeme katika maeneo yasiyokuwa na umeme ili wawadanganye wanawaletea umeme, lakini msiwape kura,” alisema.
    Ili kuthibitisha jinsi CCM walivyopoteza mwelekeo, alimtolea mfano Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Abdulrahman Kinana ambaye amekuwa akisema baraza la mawaziri lina mawaziri mizigo.
    Kutokana na hali hiyo, alisema kama angekuwa Kinana angelazimika kuihama CCM na kujiunga na Ukawa kwa kuwa ndio wenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

    MGOMBEA UBUNGE
    Naye mgombea ubunge katika Jimbo la Makambako, Mhema Oraph (Chadema), aliwaambia wananchi kwamba atakapoingia madarakani, atatatua kero ya maji, atafuta ushuru usiokuwa na maana, atasaidia upatikanaji wa umeme na pia atatatua migogoro ya ardhi iliyokithiri jimboni humo.
    Wakati huo huo, aliyekuwa Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Mkoa wa Njombe, Ally Mwimike, alitangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Ukawa.
    Ingawa hakutaja chama alichojiunga nacho katika umoja huo, Mwimike alisema Watanzania wanatakiwa kufanya mabadiliko kwa kuwa CCM imetawaliwa na rushwa.

    MWANAHALISI
     MGOGORO mpya umeibuka Ngorongoro baada ya Askari wa Wanyamapori wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kudaiwa kuwapiga wafugaji wa kata za Endulen na Alaitole wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hiyo.  
    Vurugu hizo zimeibuka mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha wafugaji 27 kujeruhiwa huku wengine 22 kuwekwa kizuizini, pamoja upotevu wa mifugo 52 ambayo haijulikani ilipo.
    Chanzo cha mgogoro huo kinaelezwa kusababishwa na baadhi ya wafugaji kupeleka mifugo yao eneo la Mash ambalo hutumiwa kunywesha mifugo yao hasa kipindi cha kiangazi, ambapo askari walipowakuta walianza kuwashambulia kwa madai kuwa hawaruhusiwi kufuga mifugo yao katika eneo hilo.
    Wafugaji hao wameeleza kuwa katika kipindi hiki cha kiangazi ambacho wanakabiliwa na uhaba wa maji hasa kwa ajili ya mifugo yao na wamekuwa na utaratibu wa kutumia eneo hilo kwa makubaliano ya kila mwaka ila kwa mwaka huu imekua tofauti kwani wamefukuzwa pamoja na kupigwa na askari hao kinyume cha sheria.
    Mzee wa mila jamii ya Wamasai, Kadogo Olduati amesema kuwa kwa kipindi kirefu wameishi katika ardhi mseto yenye mchanganyiko wa wanyamapori na mifugo pamoja na binadamu bila kusababisha athari zozote katika kwa mazingira na wanyama.
    Olduati ameitaka Mamlaka ya Ngorongoro isiegemee upande wa wanyamapori na kuwasahau wafugaji ambao hutegemea ufugaji kuendesha maisha yao ya kila siku.
    Katibu wa Baraza la Wafugaji, James Moringe ameiomba mamlaka ya Ngorongoro na Baraza la wafugaji kwa pamoja kuitisha kikao cha haraka ili kuepusha mgogoro huo ambao unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuathiri uhifadhi na utalii kwa ujumla.
    Mhifadhi wa Ngorongoro hakuweza kupatikana kuzungumzia tikio hilo kwa kuwa simu yake ya mkononi haikupatikana, lakini pia walinzi waliwazuia waandishi kuingia ofisini kwake mpaka watakapopata kibali maalum.

    NIPASHE.
     Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imepitisha rufaa 13 zilizokuwa zimewekewa pingamizi za kugombea ubunge katika baadhi ya majimbo nchini yakiwamo ya Ludewa la Deo Filikunjombe (pichani kushoto), mkoani Njombe na Bumbuli mkoani Tanga linalotetewa na Januari Makamba.
     
    Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam Ofisa wa Tume, Athumani Masesa, alisema uamuzi huo umetolewa baada ya kusikiliza rufaa 40 kati ya 56 zilizowekewa pingamizi. Makamba na Filikunjombe ni miongoni mwa wagombea waliotarajiwa kupita bila kupingwa baada ya kuwawekea pingamizi wapinzani wao, hasa kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).  
     
    Alisema tume hiyo ilitulipia mbali pingamizi nyingine  27 baada ya kupitia maelezo na kubaini kuwa hazikuwa na hoja za msingi za kuishawishi .
     
    Aliyataja majimbo mengine kuwa ni Bumbuli ambalo mgombea wake  wa CCM, January Makamba,  Peramiho la mgombea wa chama hicho, Jenister Mhagama na Ludewa la Deo Filikunjombe.
     
    Alisema Nec leo inatarajia kuendelea kupitia rufaa nyingine zilizobakia na baada ya kukamilisha kazi hiyo, wataanza kupitia  196 za madiwani kwa ajili ya maamuzi.
     
    Awali waliotangazwa kupita bila kupingwa ni Makamba, Rashid Shangazi, Abdallah Chikota(Nanyamba) na Filikunjombe.
     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: NIMEKUWEKEA HABARI KUU KATIKA MAGAZETI MBALIMBALI LEO SOMA HAPA. Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top