728x90 AdSpace

  • Latest News

    Friday, April 29, 2016

    Je Tanzania imepiga hatua kubwa Afrika mashariki kujenga daraja la kigamboni? Majibu yako hapa!


    Ni eneo la Vijibweni na Kurasini wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam, ndipo utakapolikuta daraja la kisasa linaloning’inia kwa nyaya mbalimbali ambazo kiitaalamu ndio zinazobeba uzito wa magari na watu wanaolitumia daraja hilo.

    Ukifika eneo hilo, utashuhudia mandhari ya kuvutia ya barabara za kisasa zilizopambwa na taa za rangi mbalimbali, hasa nyakati za usiku pamoja na barabara za juu zinazoelekea pande mbalimbali za jiji hilo la Dar es Salaam.

    Daraja la Nyerere ni daraja la kipekee kujengwa nchini Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, kutokana na ukweli kuwa ni daraja la kwanza kujengwa baharini lakini pia ni daraja lililojengwa kwa gharama kubwa kutokana na ujenzi wake kutumia teknolojia ya kisasa zaidi katika eneo la kuhimili uzito.

    Urefu wa daraja hilo lililopewa jina la muasisi wa Tanzania na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere ni mita 680 na upana wa mita 32, na lina barabara sita, tatu zikitoka Kigamboni kwenda Kurasini na tatu kutoka Kurasini kwenda Kigamboni. Aidha daraja hilo lina urefu wa mlazo wa kilometa mbili na nusu.

    Ukweli ni kwamba mtindo wa ujenzi wa daraja hilo ni wa kipekee katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa linakuwa daraja la kwanza kujengwa kwa mtindo wa kuning’inia ambao kwa lugha ya kitaalamu unaitwa ‘cable stayed bridge’. Kumalizika na kuanza kutumika rasmi kwa daraja hilo, kunahitimisha usemi maarufu unaosema hakuna marefu yasiyo na nchi na waswahili husema ‘hayawi hayawi sasa yamekuwa’.

    Hii ni kutokana na ukweli kwamba daraja hilo limekuwa likisubiriwa kwa hamu na wakazi wa Dar es Salaam hususani wa maeneo ya Kigamboni kwa muda mrefu.

    Historia ya ujenzi wa daraja hilo, inaanzia miaka mingi iliyopita 1930s ambapo kumekuwepo na mipango na mikakati ya kujenga daraja hilo ikiwa ni moja ya njia ya kuwarahisishia wakazi wa ‘kisiwa’ hicho cha Kigamboni usafiri wa kufika eneo la katikati ya jiji la Dar es Salaam.

    Pamoja na kwamba ujenzi wa daraja hilo ulionekana kama ndoto isiyotimia hasa kutokana na ukosefu wa fedha wa Serikali na suala lenyewe kuchukua muda mrefu, sasa hali imebadilika kwani tayari ujenzi wake uko katika hatua za mwisho lakini matumizi ya daraja hilo, yameshafunguliwa rasmi.

    Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa Ujenzi wa daraja hilo la Nyerere, Mhandisi Karim Mattaka kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) daraja hilo ni imara na litaweza kudumu na kutumiwa na watanzania kwa zaidi ya miaka 100.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Je Tanzania imepiga hatua kubwa Afrika mashariki kujenga daraja la kigamboni? Majibu yako hapa! Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top