Kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ujerumani na klabu ya Arsenal ya
England, Mesut Mustafa Ozil, yu mbioni kusaini mkataba mpya ambao
utamuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni laki mbili (200,000) kwa juma.
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger ana matumaini makubwa ya
kukamilishwa kwa dili hilo, kutokana na fununu zinazoendelea kumuhusu
Ozil kuhitajika kwenye klabu nguli za barani Ulaya kama Juventus pamoja
na FC Bayern Munich.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, kwa sasa analipwa mshahara wa
Pauni laki moja na arobaini (140,000) kwa juma, hivyo kutakua na
ongezeko la Pauni elfu sitini (60,000) katika mshahara wake kama
atakubalia kusaini mkataba mpya.
Arsene Wenger, pia anamuhangaikia, mshambuliaji wake kutoka nchini
Chile, Alexis Sanchez ili aendelee kusalia klabuni hapo kwa kuwa mbioni
kumsainisha mkataba mpya.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, amekua katika ombwe la
kuhusishwa na mipango wa kuihama The Gunners, baada ya kuchoshwa na
mwenendo uliopo klabuni hapo wa kutofikia lengo la kutwaa ubingwa wa
nchini England sambamba na kutofika mbali kwenye michuano ya ligi ya
mabingwa barani Ulaya.
0 comments:
Post a Comment