Beki Hassan Kessy amemvaa Rais wa Klabu ya Simba, Evans
Aveva na kumwambia asipotoshe umma na badala yake awaambie ukweli
mashabiki na siyo kumtaja yeye ndiyo chanzo cha kukosa ubingwa wa Ligi
Kuu Bara msimu huu.
Hiyo ni siku chache tangu Aveva ataje sababu ya timu hiyo kukosa ubingwa huo uliochukuliwa na Young Africans.
Beki huyo, tayari amesaini mkataba wa miaka miwili ya
kuichezea Young Africans kwa dau la shilingi milioni 40 huku akilipwa
mshahara wa shilingi milioni 2 kwa mwezi.
Kessy alisema alichokifanya rais huyo ni kumtumia kama
mwamvuli kuwafunika viongozi hao ili wasionekane kikwazo cha wao
kushindwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji hilo.
Kessy alisema kwanza kabisa aliondoka Simba ikiwa timu
hiyo imebakiza michezo mingi ambayo kama viongozi na benchi la ufundi
wangefanya kazi yake vizuri, ingechukua taji hilo, hivyo anashangaa yeye
kutajwa.
Aliongeza kuwa, viongozi hao wasiitumie njia hiyo
kumharibia kwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo huku akipanga kwenda
kuwavaa mabosi hao akidai malipo yake ya mshahara wa mwezi uliopita
baada ya kupata taarifa za malipo hayo.
“Kwanza hao viongozi wa Simba wasijisahaulishe kabisa,
wakumbuke ninawadai malipo yangu ya mshahara wa mwezi uliopita, tayari
nimeshamwambia katibu wao ninataka mshahara wangu, ni baada kutoona
fedha kwenye akaunti yangu.
“Kwa sababu hao viongozi wanajifanya wajanja, bila aibu
kabisa wanatangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mimi ndiyo sababu ya
timu kushindwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu, hivi ni kweli hicho
walichokiongea!
“Kiukweli kabisa kwanza mashabiki ni mashahidi, mimi
niliondoka Simba mapema, baada ya kuona ninatengwa na viongozi,
walifungwa mechi na Mwadui FC, nilikuwepo na walipokwenda kucheza na
Majimaji na kutoka suluhu nilikuwepo, viongozi hao hawana hoja, ni vema
wakawaambia ukweli mashabiki,” alisema Kessy.
0 comments:
Post a Comment