Kocha wa Stand United, Patrick Liewig amewatema rasmi wachezaji
watano waliokuwa kikosi cha kwanza huku akiingiza wapya watatu kutoka
mchangani.
Liewig amewatema Rajabu Zahiri, Haruna Chanongo, Nassoro Masoud
‘Chollo’, Abuu Ubwa na Salum Kamana ambao mikataba yao inamalizika
mwishoni mwa msimu huu huku akimvutia pumzi straika wake Elius Maguli
ambaye anataka kukaa naye mezani kwa ajili ya mazungumzo ya mkataba
mpya.
Liewig anasubiri Maguli arejee kutoka kwenye majaribio yake ya siku
kumi katika timu ya Amazulu ya Afrika Kusini ambako alikwenda juzi
Jumatatu, mkataba wa Maguli na Stand unamalizika mwezi Agosti. Hata
hivyo kuna uwezekano mkubwa wa Maguli kugoma kuongeza mkataba mpya kwani
hana mahusiano mazuri ya kazi na kocha wake huyo.
Wachezaji ambao mikataba yao inamalizika na wapo kwenye mipango ya
Mfaransa huyo kuongezwa mikataba mipya ni nahodha Jacob Masawe na
Seleman Selembe huku waliowasajili kutoka mchangani kupitia programu yao
maalumu kati ya Acacia na Sunderland ni kipa Charles Minza, beki wa
kati John Mtabesya na straika Adam Salamba.
Mratibu wa timu hiyo, Mbasha Matutu alisema: “Hao wachezaji wapya
wametoka kijiji cha Ilogo kinachozunguka mgodi wa Bulyanhulu, wametokana
na mpango maalumu wa wadhamini wetu kwa kushirikiana na Sunderland
ambapo lengo ni kukuza vipaji kwa vijana.
“Kuna wachezaji watakaosajiliwa wenye uzoefu, ila hao walioachwa ni
kutokana na mikataba yao kumalizika na hakuna uwezekano wa kuwaongeza
mikataba mipya kwani kocha hatakuwa na mipango nao hapo baadaye, ila
Maguli bado tunamuhitaji, akirejea tutazungumza naye ingawa kukubali au
kukataa ni hiari yake mwenyewe,” alisema Mbasha.
0 comments:
Post a Comment