Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema licha ya kupewa
vitisho kumzuia asihudhurie msiba wa aliyekuwa mkurugenzi wa jiji,
Wilson Kabwe, amezingatia ubinadamu na kuweka msimamo kuwa ataendelea
kutimiza wajibu wake.
Makonda alisema hayo jana wakati wa kuaga mwili wa Kabwe kwenye ukumbi wa Karimjee, kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwake Mamba Mpinji wilayani Same, Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayofanyika leo.
Awali, mmoja kati ya wanafamilia alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya
habari akisema kuwa familia haihitaji ushiriki wowote wa Serikali kwenye
maandalizi ya mazishi hayo.
Alitoa kauli hiyo kutokana na Kabwe kusimamishwa kazi kwa amri ya
Rais John Magufuli baada ya kusomewa makosa yake na Makonda mbele ya
umati wa watu wakati wa uzinduzi wa Daraja la Kigamboni.
Hata hivyo, ndugu wengine walikanusha kauli hiyo na kueleza kuwa
Serikali imekuwa ikishirikiana na familia katika kumuuguza Kabwe na
kwamba kifo chake hakikutokana na kusimamishwa kazi kwa kuwa wakati
uamuzi huo unatangazwa alishaanza kuugua.
Akizungumza kwenye shughuli hiyo, Makonda aliipongeza familia ya
marehemu, akisema imevuka mtihani ambao Watanzania wengi wangeshindwa
kutokana na kulivisha tukio hilo sura ya tofauti wakati wa msiba.
“Baadhi ya watu waliniambia nisihudhurie msiba na hata baadhi ya vyombo vya habari vikatengeneza mazingira vinayoyaona kwamba yanafaa,” alisema Makonda.
“Ila nitaendelea kutimiza wajibu wangu na wanafamilia mmeliona hilo na niwape pongezi.”
Makonda aliwasihi Watanzania kuwa watulivu na kushauri watumishi wa umma kuwa waadilifu katika kazi zao.“Maadam Kabwe amelala, tusitumie fursa hii kumrundikia mizigo eti
tukifikiri kwamba tutakuwa salama mbele za Mungu.
Tuhakikishe kila mmoja
anafanya kwa nafasi yake na kwa wajibu wake ili tusiwatwishe mizigo
watu waliotangulia mbele za haki.”
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi za kidini,
wafanyakazi wa umma na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Mkuu wa
Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
Akitoa salamu za Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi),
George Simbachawene alisema kifo cha Kabwe kimewasikitisha na kwamba
ameacha pengo, si kwa familia pekee bali hata serikalini.
0 comments:
Post a Comment