Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil, Carlos Dunga amemuongeza
kiungo wa klabu ya Orlando City ya nchini Marekani, Ricardo Kaka, kwenye
kikosi chake ambacho kipo katika maandalizi ya mwisho ya fainali za
mataifa ya kusini mwa Amerika (Copa America).
Dunga amemuita kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, baada ya
kumuondoa kiungo wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich,
Douglas Costa, ambaye anasumbuliwa na majeraha ya paja la mguu wake wa
kushoto.
Kaka ameongezwa katika kikosi cha Brazil na kuwa na matumaini ya
kuichezea tena timu ya taifa ya nchi yake, ambapo kwa mara ya mwisho
alifanya hivyo mwaka 2012.
Kiungo huyo ambaye aliwahi kuzitumikia klabu nguli barani Ulaya AC
Milan na Real Madrid, amekuwa mchezaji wa pili kuitwa kikosini kwa lengo
la kujazia nafasi, akitanguliwa na mshambuliaji wa klabu ya Benfica,
Jonas Gonçalves Oliveira aliyechukua nafasi ya Ricardo Oliveira.
Timu ya taifa ya Brazil, imepangwa katika kundi la pili (B) katika fainali za Copa America sambamba na Ecuador, Haiti na Peru.
Mwishoni mwa juma hili (Siku ya jumapili) Brazil itacheza mchezo wa
mwisho wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Panama katika mji wa Denver
nchini Marekani, kabla ya kuanza kwa fainali za Copa America Juni 04.
0 comments:
Post a Comment