Serikali imefuta mchakato wa kutangaza ada elekezi tangu katikati ya Mei
mwaka huu, ambapo udhibiti wa ada hizo sasa utafanywa na Kamishna wa
Elimu na Idara ya Ukaguzi.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako alisema hayo jana jioni alipokuwa akihitimisha mjadala wa
bajeti ya wizara hiyo na kuongeza kuwa mchakato huo umefungwa baada ya
kujadiliana na wamiliki na Kamati ya Bunge.
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, usimamizi wa utoaji wa michango na
ada holela katika shule hizo utashughulikiwa kwa mujibu wa sera, ambapo
kutatakiwa kuwepo kwa kibali kwanza.
Alisema kutokana na hatua hiyo ya Serikali, ambayo inalenga kupata
muda wa kutafakari suala hilo na kutafuta namna bora ya udhibiti, sasa
hakutakuwa na ada elekezi ila michango itadhibitiwa.
Awali katika mjadala, baadhi ya wabunge walipinga mchakato huo na
kutaka Serikali kujikita katika kuboresha shule zake na kuachana na
utoaji wa ada elekezi. Akizungumza katika mjadala huo, Mbunge wa
Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisema hakuna sababu ya kuwa na ada elekezi
kwa shule binafsi.
Lugola alisema kama Serikali ikitaka shule binafsi zife, ni kuwalipa
vizuri walimu wake, kuwajengea nyumba zao, kuwa na madarasa na kuweka
chakula na hayo yakikamilika, hakuna mtu binafsi atakayepandisha ada.
Kwa mujibu wa Lugola, kama hayo hayatafanyika, kila mtu ana uamuzi wa
kumpeleka mtoto katika shule anayotaka hata Ulaya.
“Kuna tatizo gani na hizi shule za binafsi? Kwanza wamerundikiwa kodi
nyingi mara kupaka rangi magari na mengineyo, sasa watarudishaje hizo
fedha? Ndiyo maana wanatoza ada kubwa,” alitetea.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Hassan (Chadema), alielezea
kushangaa ni kwa jinsi gani ada elekezi itawekwa, wakati hakuna viwango
vya utoaji elimu kwa watoto. Mbunge wa Maswa, Mashimba Ndaki (CCM),
alisema suala hilo la ada elekezi watakaonufaika ni watu wenye fedha
kwani ndiyo wanaowapeleka watoto katika shule binafsi na kusahau
kuboresha shule za Serikali ambazo ni kwa watu wenye vipato vya kawaida.
Ndaki alisema iwapo shule za Serikali zingekuwa bora, zingechukua
wanafunzi wote na zile za binafsi zingekosa wateja kwa gharama zao hizo
kubwa, hivyo hakuna sababu ya kuwawekea ada elekezi.
“Shule binafsi wanapata wateja kutokana na miundombinu mibovu,
matatizo ya walimu yanayotokana na kutotendewa haki katika shule za
Serikali tofauti na shule binafsi ambazo wanawathamini walimu na kufanya
watoe elimu bora,” alisisitiza.
Alitaka waziri, badala ya ada elekezi angekuja na mkakati madhubuti
wa kuboresha shule za Serikali kwa kuwapa mahitaji yao walimu, kununua
vitabu mashuleni na kuboresha miundombinu na shule hizo na hilo
lingesababisha wapunguze wenyewe ada zao.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Mahawe (CCM) alisema Sheria ya Elimu ya
1978, inasema elimu siyo biashara bali huduma, lakini sasa wanaotoa
elimu hiyo binafsi wanaonekana kama wao ni maadui.
Alisema shule binafsi, zinasaidia kusomesha Watanzania lakini bila
kuthaminiwa wakati nchi nyingine watu binafsi wanasaidiwa kuwalipa
mishahara, hapa nchini wanawapiga chini licha ya kuwa wanasaidia
kusomesha hata watoto yatima, ili kuondoa watoto wa mitaani huku
akieleza yeye katika shule yake anasomesha watoto 67.
Mahawe alisema shule binafsi wanalipa kodi zaidi ya 10, licha ya kuwa
wameokoa kupeleka watoto kusomeshwa katika nchi za Kenya na Uganda huku
akiomba wizara kuwapatia dawati wizarani ili wawape ushauri hususan
katika mitaala.
Mbunge huyo alilalamikia shule binafsi kutengwa na wizara kwani hivi
karibuni walitoa mafunzo kwa walimu wa watoto wa darasa la kwanza mkoani
Dodoma bila kuwashirikisha
0 comments:
Post a Comment