Jeshi la Polisi mkoani Tanga limemkamata mwanamke mmoja mkazi wa
Kijiji cha Kimamba, Kata ya Negero wilayani Kilindi, Tabu Chabai (23)
kwa tuhuma za kushirikiana na mtandao wa majambazi.
Vilevile, mtuhumiwa mwingine, Waziri Luhaya, anatafutwa na jeshi hilo kuhusiana na tukio hilo, baada ya kutoroka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Tanga, Leonard Paulo, alisema Chabai alikamatwa Mei 2, mwaka huu usiku
katika Kijiji cha Kimamba, Kata ya Negero.
Kwa mujibu wa Kamanda Paul, mtuhumiwa huyo alikamatwa polisi walipokuwa kwenye msako maalum wa wahalifu.
“Kuna taarifa kutoka kwa raia wema zilitufikia na tukaamua kwenda
nyumbani kwa mtuhumiwa huyo kufanya upekuzi na kukuta vitu mbalimbali vilivyokuwa vikitumika kwenye uhalifu.
“Mtuhumiwa huyo alikutwa na silaha mbalimbali zikiwamo bunduki tatu
za shortgun zilizotengenezwa kienyeji, bastola moja iliyotengenezwa
kienyeji, risasi za shortgun 51 na ganda moja la risasi.
“Tulikamata pia panga moja, majambia mawili, simu 14 za aina
mbalimbali, makoti matatu, kofia za kininja na shati linalodhaniwa kuwa
ni la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Vitu hivyo, vilikamatwa vikiwa vimehifadhiwa kwenye mfuko wa sulphate,” alisema Kamanda Paulo.
Kamanda alisema polisi wanaendelea kuwashikilia watu saba kuhusiana
na matukio ya uhalifu kabla hatua za sheria hazijachukuliwa dhidi yao.
“Kwa hiyo, nawaomba wananchi tuendelee kushirikiana kuhakikisha
tunawafichua wahalifu ili maeneo yetu yaendelea kuwa salama,” alisema.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Tanga, limekamata kilo 802 za
mirugi iliyokuwa ikisafirishwa kutoka Kenya kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Paulo alisema jana kwamba mirungi hiyo ilikamatwa katika
Kijiji cha Mtimbwani, Kata ya Mtimbwani wilayani Mkinga, polisi
walipokuwa kwenye operesheni ya kukabiliana na wahalifu.
0 comments:
Post a Comment