Ule msemo wa waswahili usemao “Adui Yako Muombee Njaa” umedhihirishwa
na mshambuliaji kutoka nchini Argentina na klabu bingwa Hispania FC
Barcelona, Lionel Messi baada ya kuonyesha kuwa na matumaini ya kuwaona
wapinzani wao Real Madrid wakimaliza msimu wakiwa mikono mitupu.
Messi ambaye aliiongoza FC Barcelona kupata ushindi wa kishindo wa
mabao matano kwa sifuri mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Espanyol
katika mshike mshike wa ligi ya nchini Hispania, amezungumza kauli hiyo
alipofanyiwa mahojiano na kituo cha televisheni cha ESPN cha nchini
Marekani.
Messi amesema ana imani kubwa, Real Madrid wanaonolewa na gwiji wa
soka kutoka nchini Ufaransa, Zinedine Zidane wataambulia patupu mwishoni
mwa msimu huu, licha ya kuwa katika mazingira mazuri ya kuwapa
ushindani kwenye mbio za ubingwa wa La Liga pamoja na kutinga kwenye
hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya ambapo watacheza dhidi
ya Atletico Madrid, Mei 28 huko mjini Milan nchini Italia.
“Ni kawaida kwa watu wa Barcelona kuona Real Madrid hawafanikiwi
katika msimu wowote, na mimi ni mmoja kati yao ambaye ninaamini kwa
msimu huu hawatoondoka na chohote licha ya kuwa katika mazingira mazuri
ya kuwania mataji,” Messi alizungumza katika kipindi cha ESPN
“Sisi tuna nafasi nzuri ya kushinda taji la La Liga msimu huu,
kutokana na mazingira ya msimamo wa ligi ya nchini Hispania kutubeba kwa
tofauti ya point moja na sio kwao, na nikuhakikishie hata katika ligi
ya mabingwa barani Ulaya hawatofanya lolote, kutokana na ubora wa
wapinznai wao.” Aliongeza mshambuliaji huyo anayeshikilia tuzo ya ubora
wa soka duniani
Katika mchezo wa mwisho wa ligi ya nchini Hispania msimu huu ambao
utachezwa mwishoni mwa juma hili na kuamua hatma ya ubingwa, Real
Madrid watapambana na Deportivo La Coruna huku FC Barceloan wakipambana
na Granada CF.
FC Barcelona pia watakuwa na nafasi nyingine ya kuwania taji la
mfalme msimu huu kwa kucheza dhidi ya Sevilla, mwishoni mwa juma lijalo.
0 comments:
Post a Comment