Umoja wa Wakulima wa Chai Usambara Tea Growers Association (UTEGA),
umetoa notisi ya siku 90 kwa Serikali kulipwa fidia ya Sh bilioni 17 .8
kwa kuwasababishia hasara baada ya kukifunga Kiwanda cha Chai cha
Mponde na baadaye kutangaza kukitaifisha hivi karibuni.
Madai hayo yalibainishwa katika barua yao ya malalamiko yenye
kumbukumbu namba FK/CF/UTEGA-Mponde Tea iliyowasilishwa kwa Msajiri
Hazina na nakala kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kupitia notisi hiyo iliyoandikwa na Kampuni ya FK Law Chambers ya
jijini Dar es Salaam, wakulima hao wanadai kiwanda hicho kimetaifishwa
na Serikali wakati ikitambua ilikiuza kwa mikataba rasmi kupitia Tume
ya Rais ya Ubinafisishaji Mashirika ya Umma (PSRC).
Notisi hiyo ambayo MTANZANIA ina nakala yake, Serikali kupitia
Msajiri Hazina, imetakiwa kulipa fidia ndani ya siku 90 tangu tarehe ya
notisi hiyo na kwamba gharama zitaendelea kuongezeka wakati
kesi ikiendelea mahakamani.
Katika notisi hiyo yenye kumbukumbu FK/UTEGA-Mponde Tea/Claims ya Mei
4, mwaka huu kusudio lao la kwenda mahakamani ni kujadili hoja mbili
kubwa za kisheria.
UTEGA kupitia FK Law, wanadai kitendo alichokifanya Msajiri wa Hazina
cha kutaifisha kiwanda hicho, huku akitambua wanayo hati halali ya
umiliki wa ardhi ni kinyume cha kifungu cha 3(1) (b),(f) na (g) cha
sheria ya ardhi sura ya 113 ya sheria za Tanzania iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002 inayosomeka pamoja na vifungu 3,4,6,7,8 na 12 vya
sheria ya utaifishaji Na.12 ya mwaka 1968 (iliyofanyiwa marekebisho)
sura ya 118 ya sheria za Tanzania mwaka R.E. 2002 (the land Acquisition
act).
Kwa msingi huo, UTEGA wanataka walipwe hasara zote zilizotokea
kutokana na Serikali kutosimamia sheria za nchi hasa baada ya kuvamiwa
huku ikitambua kuwa wanacheti cha uwekezaji nchini kutoka Kituo cha
Uwekezaji (TIC).
Hasara hizo, ni pamoja na mali zote zilizonunuliwa na UTEGA kutoka
kwa Serikali na zile walizonunua kwa ajiri ya kuendeleza uwekezaji huo
ikiwa na gharama za uendeshaji zilizotokana na kiwanda kusimamishwa
kikiwa kinafanya uzalishaji.
Hasara nyingine, ni za kupunguza wafanyakazi na kuwalipa mishahara
yao, posho na malipo mengine wanayostahili, gharama za kuchukua hatua za
kisheria kuhusiana CHC, Serikali, wizara,mkoa na mamlaka nyingine za
Serikali.
Kutokana na hasara hizo na nyingine, Mponde Tea na UTEGO na Lushoto
Tea wamepata hasara ya Sh 7,824,764,219 kwa kupoteza uwekezaji kutoka
benki ya NMB.
Pia wanadai wamepoteza uanachama katika shamba la chai Lushoto na
wilayani Korogwe, hali iliyosababisha kupoteza soko la chai ambalo
angeweza kupata Sh bilioni 10 hivyo wanaidai Serikali kulipa fidia ya
kiasi hicho cha fedha.
Ingawa sababu ya Msajiri wa Hazina anasema alikitaifisha kiwanda
hicho kutokana na UTEGA kushindwa kulipa deni la Sh milioni 350
lililokuwa limebaki, FK Law Chambers wanasema wateja wao walishaeleza
sababu ya kutolipa deni hilo ni kunyang’anywa kwa shamba la miti la
Sakare na kwamba walikuwa wakisubiri kurejeshewa shamba hilo ndipo nao
walipe kwani sehemu ya fedha walizolipa kununua kiwanda inahusisha
shamba hilo kama mkataba wa mauziano unavyosema.
“Kuthibitisha hilo UTEGA waliandika barua Februari 21,2011 ya kusudio
la kuishtaki Serikali (initial notice of intention to sue the
government) licha ya kupokelewa serikalini si Consolidated Holdings
Limited (zamani PSRC) wala Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyejibu notisi
hiyo,” wanasema FK Law Chambers kwa niaba ya wateja wao.
Notisi ya UTEGA kuishitaki Serikali,imenakilishwa ofisi ya Waziri
Mkuu, ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Katibu Mkuu wa
Viwanda na Biashara na Uwekezaji, na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, na
Ushirika, kusudio hilo linatokana na kifungu cha sita cha mwenendo wa
Serikali kama walivyofafanua katika notisi yao.
Katika kusudio hilo,kampuni hiyo inasisitiza hoja ya kwanza inahusu
mkataba wa mauziano wa Desemba 7, 2007 kati ya Serikali iliyowakilishwa
na Kamati ya Rais ya Kubinafsisha Mashirika ya Umma (Presidential
Parastatal Sector Reform Commission-PSRC) na Umoja wa Wakulima wa Chai
Usambara (UTEGA).
“Hoja ya pili ni barua ya kusitisha na kutaifisha mali zote za
Kiwanda cha Mponde (the Letter of Termination and Repossession)
iliyoandikwa Januari 22 mwaka huu na Msajiri wa Hazina dhidi ya UTEGA
“Katika hoja hii Msajiri wa Hazina na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndio walengwa wakuu katika madai haya.
“Kwenye mkataba huo wa mauziano, Serikali iliyowakilishwa na PSRC
inatajwa kama muuzaji (vendor) na UTEGA wanatajwa katika mkataba huo
kama wanunuzi (Purchaser) kama ilivyofafanuliwa katika kifungu cha pili
cha mkataba huo.
FK Law wanadai pia kuwa katika hati ya makubaliano (MoU) ya Novemba
22,1999 kati ya PSRC na UTEGA, Serikali ilikubali kuuza mali zote za
Mponde Tea Estate yakiwamo mashamba ya chai, kiwanda, majengo, shamba la
miti la Sakare na nyumba za wafanyakazi zilizopo katika Kiwanja Na.2
Mpalalu Lushoto na Serikali kukabidhi hati ya Kiwanja hicho Na.5609
ambazo kabla ya kuuzwa zilikuwa chini ya Mamlaka ya Chai Tanzania (TTA).
Katika notisi hiyo, inadai baada ya mauziano hayo, UTEGA walipata
mbia wao ambaye ni Lushoto Tea Company Limited, waliyeingia naye mkataba
wa uwezeshaji ili kupatikana fedha za kuendesha kiwanda hicho na hati
ya makubaliano kati ya UTEGA na Lushoto Tea Company Limited, ambapo
UTEGA inamiliki hisa asilimia 50 na zilizobaki ni za mbia. Hati hiyo
ilipelekwa kwa PSRC ambao waliridhia makubaliano ya wawili hao.
FK Law wanaeleza pia kuwa wateja wao baada ya kupata nyaraka zote za
kuwahalalisha zikiwemo leseni mbalimbali walifanya uwekezaji uliofikia
Sh bilioni 2.3 na walikubaliana kuanzisha kampuni ya pamoja
itakayosimamia shughuli zote iliyoitwa Mponde Tea ambayo baadaye iliomba
mkopo wa Sh bilioni 2 kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya ukarabati,
uboreshaji na upanuzi wa kiwanda hicho.
January 2008, notisi hiyo inaeleza kundi la watu wasiojulikana
walivamia shamba la miti la Sakare lililokuwa likitumika kukata kuni za
kuendeshea kiwanda, shamba ambalo liliuzwa na Serikali kwa UTEGA kama
sehemu ya mali za kiwanda hicho na Serikali ikaacha kuwachukulia hatua
wavamizi hao wala haikutaka kuwaondoa licha ya kujua shamba hilo
lilishauzwa kwa UTEGA.
MTANZANIA lilimtafuta Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru ili kujua
iwapo amepokea notisi ya Serikali kushtakiwa mahakamani, alisema mpaka
jana alikuwa hajaipokea.
“Sijaipata hiyo hati (notisi)… waache wadai, hawanidai mimi, wanaidai
Serikali si wanaamini kwamba haki itapatikana huko mahakamani…. ‘Let
them do it’,” alisisitiza Mafuru.
source;Mtanzania.
0 comments:
Post a Comment