Dawa za kutibu binadamu zinazomilikiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD),
zimegundulika kuuzwa katika duka moja la mfanyabiashara binafsi lililoko
eneo la Mwananyamala kinyume na agizo la Serikali.
Hayo yalibainika wiki iliyopita baada ya mwandishi wa habari na
mhariri sanifu wa gazeti hili, Dennis Luambano, kwenda katika Duka la
Damaco lililoko nje ya Hospitali ya Mwananyamala na kununua dawa zenye
nembo ya MSD huku akinyimwa risiti za kodi zinazotambuliwa na Mamlaka ya
Mapato (TRA) na kupatiwa iliyoandikwa kwa mkono.
Akizungumzia tukio hilo katika chumba cha habari cha gazeti la
Mtanzania, Sinza Kijiweni, Luambano alisema dawa hizo zinauzwa kinyemela
kwa wauzaji kutowapa risiti wanunuzi na kwamba mmiliki wa duka hilo
anatumia nguvu ya fedha kuficha uovu anaoufanya.
Luambano alisema baada ya kununua dawa hizo na kuanza kuhoji dawa za
Serikali kuuzwa katika duka binafsi, alikamatwa na polisi waliokuwa na
mmiliki wa duka hilo aliyemtaja kwa jina la Herman Manyanga na
kubambikiwa kesi ya ujambazi na utapeli.
“Asubuhi ya Aprili 18, mwaka huu mtoto wangu, Bahati alipata ajali ya
gari akiwa na wenzake eneo la Bamaga karibu na Kituo cha Sayansi.
Akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kupata matibabu.
“Pale Mwananyamala daktari alinielekeza kwenda kununua dawa duka la
hospitali lakini baadhi ya dawa hizo hazikuwepo ikanilazimu kwenda
kununua nje. Nilikwenda duka la Damaco lililoko nje ya hospitali na
cheti cha daktari na kuuziwa ‘urine bag, catheter na dripu’ tatu zenye
nembo ya MSD lakini muuzaji akaninyima risiti ya TRA, nilipong’ang’ania
akinipa ya kuandika kwa mkono,” alisema Luambano.
Alisema wakati akirejea wodini aliwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa
MSD, Laurean Bwanakunu, kuhusu dawa hizo ambaye alimtaka azipige picha
pamoja na risiti kisha amtumie kupitia kwenye simu yake ya kiganjani kwa
ajili ya ufuatiliaji jambo ambalo alilitekeleza kisha akarudi wodini.
Luambano alisema baadaye mwanaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kwa matibabu zaidi hivyo aliondoka na dawa zilizosalia
alizonunua kwenye duka la Damaco na kuendelea na uchunguzi wa suala hilo
ambalo Bwanakunu alieleza kuwa ametoa maagizo kwa watendaji wake
kulifanyia uchunguzi kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Chakula
na Dawa Tanzania (TFDA).
“Katika kufuatilia habari hiyo nilimtafuta mmiliki wa duka la Damaco
kupitia simu ya kiganjani ili nipate maelezo yake na yeye alisema
limemshtusha hivyo hawezi kuliongelea kwenye simu, akanitaka niende
dukani kwake jambo ambalo sikuliafiki bali nilimwalika yeye ofisini
kwake lakini alisita na kuomba nichague sehemu nyingine aje azione hizo
risiti kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua.
“Sikuona tatizo, nikamwelekeza eneo ninaloishi ni Mikocheni akasema
atafika, alikuja kweli akaniita Baa na Restaurant ya MRC iliyo jirani tu
na kwangu nikaenda kumuonyesha risiti na dawa hizo pamoja na kupata
maelezo yake.
“Alipoziona dawa na risiti alitaharuki huku akisema hata mwandiko
kwenye risiti ameshaujua hivyo akaaga kwenda dukani kwake kutafuta
ukweli kabla ya kunipa maelezo yake,” alisema Luambano.
Akisimulia zaidi sakata hilo, alisema Manyanga alimpigia simu baadaye
akimtaka wakutane saa 10 jioni siku hiyo hiyo katika Baa na Restaurant
ya MRC kwa ajili ya kumpa maelezo yake lakini alipofika aliwekwa chini
ya ulinzi wa askari polisi ambao walimfunga pingu huku wakimtuhumu kwa
ujambazi.
“Nilikwenda na kumkuta yuko amekaa peke yake. Kabla sijakaa wakaja
vijana wawili wakatoa pingu wakanifunga huku wakinieleza kuwa wameambiwa
na Manyanga mimi ni jambazi hivyo wakanipeleka kituo cha polisi
Oysterbay na kuniweka ndani,” alisema.
Alilaumu kuwa aliwekwa rumande bila kuchukuliwa maelezo hadi
alipotolewa na mkuu wa kituo ambaye pia aliitisha jalada alilofunguliwa
na baada ya kulipitia aliwaamuru askari wachukue maelezo yake kisha
wampe dhamana.
“Kabla sijatoa maelezo niliuliza kosa langu nikaambiwa ni jambazi. Jalada langu lilipewa namba OB/RB/7795/2016,” alisema.
RPC Fuime ashangaa
Luambano alieleza zaidi kuwa alifika tena kituo cha polisi Oysterbay
siku iliyofuata akiwa ameandamana na wahariri wawili wa Gazeti la
Mtanzania aliowataja kuwa ni Ratifa Baranyikwa na Charles Mullinda ambao
baada ya kushindwa kuonana na mpelelezi ya kesi hiyo walikutana na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni (RPC), Christopher Fuime ambaye
baada ya kusikiliza sakata hilo alishtuka na kuagiza polisi kufanya
uchunguzi kuhusu dawa za Serikali kuuzwa mitaani.
“Hivi MSD wanashindwaje kumkamata mtu anayeuza dawa za Serikali
wakati risiti na kidhibiti cha dawa kipo? Wanataka nini tena wakati
jambo hili liko wazi? Na mnaona jinsi wananchi wanavyolichezea Jeshi la
Polisi, huyu bwana amegundua kuwa amefanya kosa atalipuliwa amekimbilia
polisi kuja kubambikia kesi mwandishi, sasa uongo wa aina hii ndio
polisi wakichukua hatua wanalaumiwa.
“Nimewaagiza vijana wangu kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu jambo
hili kwa sababu jalada lipo hapa kwetu na sisi bwana ni kazi tu,
tutachukua hatua haraka na wananchi watajua,” alisema Kamanda Fuime.
Wakati Kamanda Fuime akitangaza kuchukua hatua za haraka kuhusu suala
hilo, Mkurugenzi Bwabakunu alisema bado uchunguzi wao unaendelea.
Alipoulizwa Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, iwapo taasisi hiyo
inalifanyia kazi suala hilo alisema limekwishafikishwa mezani kwake na
linafanyiwa kazi kwa kushirikiana na MSD.
0 comments:
Post a Comment